Mamlaka Sudan warejesheeni wananchi huduma ya intaneti-Wataalamu wa haki za binadamu

8 Julai 2019

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi wamezipinga hatua iliyochukuliwa na mamlaka nchini Sudan za kuzima mtandao wa intaneti wakisema inabana uhuru wa kujieleza na kujumuika. 

Wataalam hao wamesema “Katika wiki chache zilizopita, tumeendelea kupokea ripoti kuhusu kufungwa kwa intaneti na mitandao ya kijamii kunakofanywa na baraza la kijeshi la mpito.Uzimwaji wa intaneti ni ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa wa haki za binadamu na hauwezi kuhalalilishwa kwa mazingira yoyote yale. Tunazisihi mamlaka kurejesha haraka huduma ya intaneti. Baraza la haki za binadamu pia limelaumu hatua ambazo kwa makusudi zinazuia au kuingilia watu kupata taarifa za mtandaoni na lilizitaka nchi zote kuacha hatua hizo.”

Wakizingatia kuwa maandamano ya amani ya kudai demokrasia yakiendelea nchini humo, wataalamu hao wa haki za binadamu wameeleza kuwa kufungwa kwa intaneti kunaathiri haki za binadamu za watu wa Sudani.

“Uzimwaji wa intaneti unabana haki ya watu wa Sudani kujieleza na kujumuika na unazuia maandamano yanayoendelea.” Wataalamu hao wamesema na kuongeza, “huduma ya intaneti imekuwa ikifungwa mara kadhaa tangu kuanza kwa mwaka huu, mara ya mwisho tarehe 10 ya mwezi juni siku chache baada ya vikosi vya usalama kuyatawanya kwa fujo maandamano ya amani na kuwaua pia kuwajeruhi zaidi ya waandamanaji mia moja.”

Wataalamu hao pia wamefafanua kuwa huduma za kupata taarifa na kuwasiliana ni muhimu  wakati wa maandamano na kuwa uzuiaji wa upatikanaji wa intaneti siyo tu unaathiri haki za binadamu za kujieleza, kukusanyika na kujumuika bali una athari kubwa kwa mahitaji ya waandamanaji kwa kuzingatia haki ya kiuchumi na kijamii.

Ripoti zinasema mtandao wa intaneti unaohudumu nchini Sudan wa Zain-SDN ulichangia kwa kiasi kikubwa kukosekana kwamitandao ya kijamii baada ya kufungwa ukifuatiwa na mitandao mingine kama MTN, Sudatel na Kanartel.

Wataalamu wa haki za binadamu wamesema wako tayari kutoa msaada wowote kwa mamlaka kuhusu jambo hilo.

 

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter