Wakimbizi na wahamiaji wako katika hali mbaya kwenye vizuizi Marekani- Michelle Bachelet

8 Julai 2019

Kamishina Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet hii leo jumatatu mjini Geneva Uswisi amesema ameshangazwa na hali waliyonayo wakimbizi na wahamiaji, watoto na watu wazima wanaoshikiliwa katika vizuizi nchini Marekani baada ya kuvuka mpaka akisisitiza kuwa watoto hawapaswi kushikiliwa katika vituo vya uhamiaji wala kutenganishwa na familia zao.

Bi Bachelet amesema taasisi mbalimbali za Umoja wa Mataifa zinazohusika na haki za binadamu zimeona kuwa kuwaweka watoto wahamiaji vizuizini kunaweza kusababisha ukatili, unyama au kufanyiwa vitendo vinavyokatazwa na sheria za kimataifa, “kama daktari wa watoto lakini pia mama na kiongozi wa zamani wa nchi, nimeshitushwa sana kuwa watoto wanalazimishwa kulala sakafuni katika vituo vilivyofurika watu bila kuwa na chakula wala huduma za afya na pia katika hali duni ya mazingira ya kujisafi.”

Bi Bachelet ameendelea kueleza kuwa vizuizi vya uhamiaji havijawahi kuwa na faida kwa mtoto, “kumweka mtoto kizuizini kwa muda mfupi hata katika hali nzuri kunaweza kuwa na matokeo mabaya katika afya na makuzi yao. Fikiria uharibifu unaofanywa kila siku kwa kuruhusu hali hii ya kutisha kuendelea.”

Akizungumzuia ripoti mbaya ya kitengo cha usalama wa ndani wa Marekani kuhusu hali ya vituo vya wahamiaji kwenye mpaka wa kusini, Bachelet ameziomba mamlaka kutafuta njia nyingine za kushughulika na wahamiaji na wakimbizi watoto pia watu wazima pasipo kuwashikilia katika katika vitu.

“Kunyang’anya  uhuru wa wakimbizi na wahamiaji watu wazima kunatakiwa suluhu ya mwisho,” amesema Bi Bachelet akisisitiza kuwa hata kama hali ya kuwaweka watu kizuizini itatokea basi iwe ya muda mfupi sana ikiwa katika mchakato wa kuwalinda na katika hali yenye viwango vya kimataifa vya haki za binadamu.

“Marekani wanayo haki ya kuamua kuhusu masharti ya watu wa nchi nyingine kuingia na kukaa nchini lakini ni wazi uendeshaji katika mipaka unatakiwa kuendana na wajibu wa haki za binadamu na haitakiwi kujikita katika sera zinazolenga kuwakamata kuwashikilia na kuwarewarejesha walikotoka.” Ameongeza akisema, “katika visa vingi, wahamiaji na wakimbizi wanakuwa wamepitia katika safari za hatari na watoto wao katika kusaka ulinzi na utu wakikimbia vurugu na njaa. Wanapoamini wamefika katika usalama, wanajiukuta wametenganishwa na wapendwa wao na wamefungiwa katika hali mbaya. Hili halitakiwi kutokea popote.”

 Ofisi za haki za binadamu za Umoja wa Mataifa nchini Mexico na Amerika ya kati zimeonesha ukiukwaji wa haki kadhaa za binadamu kwa wakimbizi na wahamiaji wawapo njiani ikiwemo matumizi makubwa ya nguvu, kuwanyima uhuru bila kufuata utaratibu, kuzitenganisha familia, kuwanyima haki ya kupata huduma na pia kuwatawanya.

Hata hivyo Bachelet amewapongeza wale ambao wamekuwa wamekuwa wakiwasaidia wakimbizi na wahamiaji kwa kuwapatia huduma za msingi kama vile maji, chakula, makazi bora na misaada mingine kama hiyo.

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud