Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 10 tu ya wafanyakazi hupokea karibu nusu ya malipo yote duniani- ILO

Mwanamke akipalilia matunda Afrika Kusini.
World Bank/Samson
Mwanamke akipalilia matunda Afrika Kusini.

Asilimia 10 tu ya wafanyakazi hupokea karibu nusu ya malipo yote duniani- ILO

Ukuaji wa Kiuchumi

Utafiti wa shirika la kazi ulimwenguni, ILO unaonyesha kwamba ukosefu wa usawa ni wa viwango vya juu katika ulimwengu wa kazi.

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti huo wa ILO uliotolewa leo ukitokana na utafiti wa kitaifa, kikanda na kimataifa, asilimia 10 ya wafanyakazi hupokea asilimia 48.9 ya idadi yote ya malipo kimataifa wakati asilimia 50 ya wafanyakazi ambao wanapokea mshahara mdogo kabisa wanapata asilimia 6.4.

Ripoti hiyo ya kwanza kabisa ya ILO inaonyesha upungufu wa ukosefu wa usawa katika mapato kimataifa tangu 2004. 

Hata hivyo, hii si kutokana na kupungua kwa ukosefu wa usawa ndani ya nchi katika kiwango cha kitaifa, ukosefu wa usawa unaongezeka bali ni kwa sababu ya kuendelea kuimarika chumi zinazoibukia ikiwemo China na India.

Takwimu zinaoneysha kwamba kimataifa, pato la kitaifa linalowafikia wafanyakazi limepungua kutoka 53.7 mwaka 2004 hadi 51.4 mwaka 2017 ambapo ILO imesema ongezeko la mapato ya watu tajiri huendana na hasara kwa wengine ikiwemo wenye kipato cha wastani na kipato cha chini.

Ripoti ya ILO imesema kiwango cha mshahara wanaopokea kundi la kipato cha wastani aslimia 60 ya wafanyakazi wote kilipungua mwaka 2014 na 2017 kutoka 44.8 hadi 43 na wakatia huo huo kiwango cha wanachopokea wanaolipwa mshahara mkubwa kiliongezeka kutoka asilimia 41.3 hadi 53.5. 

Miongoni mwa nchi ambazo wanaopokea mshahara wa juu mshahara uliongezeka ni Ujerumani, Indonesia, Italia, Pakistan na Uingereza an Marekani.

Kwa upande wake nchi maskini huwa na idadi kubwa ya ukosefu wa usawa wa malipo hali ambayo inaimarisha madhila ya walio hatarini. 

Kusini mwa jangwa la Sahara, asilimia 50 ya wafanyakazi wanaolipwa mshahara mdogo wanapokea asilimia 3.3 ya kipato cha kazi ikilinganishwa na Muungano wa Ulaya ambapo kundi hilo hupokea asilimia 22.9 ya Jumla ya pato la wafanyakazi.

ILO imesema idadi kubwa ya wafanyakazi wanapokea mishahara midogo na kuwepo na kazi kwa wingi haimaanishi kuwa na kiasi toshelezi cha kukidhi mahitaji.

Pato la wastani la nusu ya wafanyakazi wanaopokea kipato cha chini ni dola 198 kwa mwezi na asilimia 10 ya wafanyakazi wanahitaji kufanya kazi kwa zaidi ya karne tatu kufikia pato sawa na aslimia 10 ya watu tajiri kwa mwaka.