Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benki ya dunia yaneemesha wakulima wa matunda Sierra Leone

Watoto wakiuza matunda kwenye soko  moja mjini Korhogo, Kaskazini-magharibi mwa Côte d’Ivoire
© UNICEF/Frank Dejongh
Watoto wakiuza matunda kwenye soko moja mjini Korhogo, Kaskazini-magharibi mwa Côte d’Ivoire

Benki ya dunia yaneemesha wakulima wa matunda Sierra Leone

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Mradi wa benki ya dunia wa kusaidia makampuni na wananchi kukua kiuchumi kutokana na biashara umeleta neena kubwa kwa wananchi wa Freetown nchini Sierra Leon ambako asilimia 80 ya biashara za nchi hiyo zinafanyika hapo.

Hapa ni katikati ya mji wa Freetown mji ambao ni kitovu cha biashara nchini Siaerra Leone. Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi na makampuni wameweka mkakati wa kuhakikisha wanaendeleza na kukuza biashara mjini humo  ziwe ndogo ama kubwa na lengo hilo linafanikiwa kwa msaada wa Benk ya Dunia . Sasa kiwanda pekee kikubwa cha maji ya matunda cha kampuni ya Sierra Agra kinashamiri na wakulima wa eneo hilo kufaidika kama anavyosema meneja wa usambaji wa kampuni hiyo Abdulai Bangura

“Hapa katika kampuni ya Sierra Agra tunafanyakazi na wakulima zaidi ya 3500, tunakusanya kutoka kwao maembe, mananasi na nazi na tunavitayarisha hapa kiwandani, tunatengenezea maji ya matunda “

Tangu mwaka 2017 Sierra Agra kimekuwa ndio kiwanda pekee kinachosafirisha hadi Ulaya maji ya matunda asilia, meneja wa usambazji anasema wanajivunia hilo na pia

“Tunaona fahari kwani sehemu kubwa ya uongozi na wafanyakazi wetu wanatoka Sierra Leone, usawa wa kijinsia ni muhimu sana kwetu na ukweli ni kwamba asilimia 90 ya wakulima tunaofanya nao kazi ni wanawake.”

Bandari ya Freetown ndio kiungo kikubwa cha usafirishaji wa biasahra ndani na nje ya Sierra Leone, lakini pia kupokea bidhaa toka nje ikiwemo Ulaya na Marekani lakini haikuwa rahisi hapo awali

“Tulikuwa tunakabiliwa na changamoto kubwa , magari yetu yalikuwa yanakaa kwenye foleni kwa saa hata siku kadhaa wakati mwingine. Mchakato wa nyaraka nao ulikuwa mgumu lakini sasa hali imeanza kutengamaa kwa sababu ya uboreshaji.”

Naye mratibu katika wizara ya viwanda na biashara nchini humo Saffie Tarawally anasema kamati ya kitaifa ya biashara na uwezeshaji inajumuisha sekta zote za umma na binafsi  katika mchakato huu na jukumu lao ni kufanya biashara kuwa ya haraka, rahisi na gharama nafuu kwa faida ya Wasierra Leone wote.