Mahali alipozaliwa Yesu mjini Bethlehem paondolewa katika maeneo ya urithi wa dunia yaliyoko hatarini.

2 Julai 2019

Kamati ya  urithi wa dunia inayokutana mjini Baku, Azerbaijan tangu Juni 30 Mwaka huu, hii leo imeamua kuliondoa katika maeneo ya urithi wa dunia  yaliyo katika hatari, Kanisa la mwanzo ambako inasadikiwa alizaliwa Yesu huko mji wa Palestina, wa Bethlehem  ulio kusini mwa Yerusalem.

 

Kamati hiyo iliyoko chini ya shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO,  imesema maamuzi yake yametokana na kazi ya ubora wa hali ya juu iliyofanywa kwenye ukarabati wa kanisa hilo, katika paa lake, ukuta wake wa mbele sehemu ya nje, mapambo yake na milango. 

Kamati pia imepokea usitishaji wa mradi wa kuchimba njia ya ardhini chini ya mzunguko ulioko katika eneo la karibu na kanisa hilo.

Kanisa hilo la mwanzo na njia ya mahujaji mjini Bethlehem, katika ukingo wa Magharibi, liko kilomita 10 kusini mwa Yerusalem katika eneo ambalo tangu karne ya pili, limekuwa likitambuliwa katika utamaduni wa kikiristo kama eneo alilozaliwa Yesu. 

Eneo hilo likiwa limewekwa katika orodha ya turathi za dunia tangu mwaka 2012, liliongezwa pia katika maeneo ya urithi wa dunia yaliyoko hatarini kutokana na kuwa katika hali mbaya.

Orodha inayoonesha maeneo ya turathi ya dunia yaliyoko katika hatari, inalenga kuifahamisha jumuiya ya kimataifa juu ya hali inayotishia hali ya awali iliyofanya eneo kuingizwa katika orodha ya urithi wa dunia.

Mkutano huo wa 43 wa kamati ya urithi wa dunia unaendelea hadi Julai 10 mwaka huu 2019.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud