Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugonjwa wa homa ya nguruwe unaendelea kusambaa Asia-FAO

Homa ya nguruwe ambayo inaambukiza sana na inaweza kuwa na athari kubwa kwa wafugaji wadogo. (Maktaba Machi 2017)
IAEA/Laura Gil Martinez
Homa ya nguruwe ambayo inaambukiza sana na inaweza kuwa na athari kubwa kwa wafugaji wadogo. (Maktaba Machi 2017)

Ugonjwa wa homa ya nguruwe unaendelea kusambaa Asia-FAO

Afya

Ugonjwa wa homa ya nguruwe au African Swine Flu, ASF,  unaoathiri nguruwe unaendelea kuenea Asia mashariki na kusini mashariki na kuweka hatarini mfumo wa kuingiza kipato na uhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu hususan wakulima wanaofuga nguruwe.

Katika taarifa yake, shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limesema ugonjwa huo unaweza kuambukiza kwa njia ya moja kwa moja au vinginevyo kufuatia ukaribu na nguruwe walioathirika na huenda ukashuhudiwa kwa muda mrefu kwenye mazingira na kwenye bidhaa zitokanazo na nguruwe.

FAO imesema tangu kuripotiwa kwa mlipuko wa ugonjwa huo mnamo Agosti mwaka jana 2018 katika jimbo la kaskazini mashariki la Liaoning, nchii China, ugonjwa umesambaa na sasa umefika katika majimbo yote ya nchi.

FAO imesema zaidi ya nguruwe milioni 1.13 wamechinjwa katika juhudi za kukabiliana na kusambaa kwa ugonjwa ambapo licha ya hatua zilizochukuliwa na serikali ya China, ugonjwa wa homa ya nguruwe umeendelea kusambaa huku sababu kuu ikitajwa kuwa ni aina ya ufugaji wa wafugaji wadogo wadogo ambao mara nyingi hukosa mbinu muafaka za kukabiliana na athari kama hizo.

Ugonjwa huo wa homa ya nguruwe licha ya kwamba hauna athari kwa bindamu husababisha homa kali kwa nguruwe, kutoka damu katika viungo na huenda ukasababisha maafa ya asilimia 100 kwa nguruwe walioathirika katika kipindi cha wiki chache kwa sababu hakuna tiba wala  chanjo ya kuzuia ugonjwa huo.

Kufikia sasa ugonjwa wa homa ya nguruwe umeripotiwa nchini Viet Nam, Cambodia, Mongolia, Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea na Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Laos ambako mamilioni ya nguruwe wamekufa au kuchinjwa ili kuzuia maambukizi zaidi.