Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viwango vya joto Ulaya vikiwa si vya kawaida, WMO yaingiwa hofu na afya ya wachezaji Afcon

Viwango vya joto barani Ulaya na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Afrika ni vya juu na vinatishai afya za binadamu, kilimo na mazingira
WMO Video screen shot
Viwango vya joto barani Ulaya na baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa Afrika ni vya juu na vinatishai afya za binadamu, kilimo na mazingira

Viwango vya joto Ulaya vikiwa si vya kawaida, WMO yaingiwa hofu na afya ya wachezaji Afcon

Tabianchi na mazingira

Shirika la hali ya hewa duniani, WMO limetoa tathmini  ya mkondo joto unaopiga maeneo ya Ulaya na baadhi  ya maeneo ya kaskazini mwa Afrika likisema kuwa viwango vya joto vilikuwa vya juu lakini maonyo ya mapema yamesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na joto la kupindukia.

Msemaji wa WMO mjini Geneva, Uswisi, Claire Nullis akizungumza na waandishi wa habari hii leo amesema kuwa, “viwango vipya vya joto ambavyo ni vya juu zaidi kuwahi kufikiwa vimetikisa Ulaya, na kutishia afya ya binadamu, kilimo na mazingira.”

Hata hivyo Bi. Nullis amesema, “ni mapema mno kuhusisha mkondo joto na mabadiliko ya tabianchi, lakini hali ya sasa inalandana na mazingira ya tabinachi ambayo yanatabiri kujirudiarudia kwa hali kama hii na hali ya joto kadri ambavyo hewa chafuzi zinaongezeka na kuchochea ongezeko la joto duniani.”

Ametolea mfano kituo cha ufuatiliaji wa viwango vya joto kitaifa nchini Ufaransa kilichopo Gallargues-le-Montueux ambacho tarehe 28 mwezi uliopita wa Juni kilirekodi nyuzi joto 45.9 katika kipimo cha selsiyasi, na vituo vingine viwili vilivyorekodi nyuzi joto 45, viwango ambavyo ni vya juu zaidi kuwahi kurekodiwa katika zama za sasa.

“Kiwango cha nyuzi joto 45.9 katika kipimo cha selsisyaji, unatarajia kukipata mwezi Agosti huko Furnace jimboni California nchini Marekani, eneo ambalo linashikilia rekodi ya zamani kabisa yam waka 1913 ya kuwa na kiwango cha juu cha joto zaidi,” amesema Bi. Nullis.

Hali ya joto kali pia imeripotiwa Hispania, Austria, Uswisi na Ujerumani.

WMO inaonya kuwa kiwango cha juu cha joto kinaweza kuambatana na ukame katika baadhi ya maeneo ya Ulaya Mashariki huku radi za mara kwa mara zinaweza kukumba maeneo ya Ulaya ya Kati na Kusini-mashariki.

Katika bara la Afrika nako maeneo ya Kaskazini nako viwango vya joto viliripotiwa kuwa juu ya nyuzijoto 40 kwenye kipimo cha Selsiyasi.

“Tuna wasiwasi mkubwa juu ya afya na ustawi wa wachezaji kwenye mashindano ya mataifa ya Afrika yanayoendelea nchini Misri kwa kuzingatia madhara ya joto kupita kiasi,” imesema WMO.

Joto na Afya

Kwa hivi sasa barani Ulaya, mamlaka za kitaifa za hali ya hewa zinashirikiana na mamlaka za utawala kitaifa na kimitaa kuweka mipango ya kuepusha madhara ya afya yatokanayo na joto.

Kwa mujibu wa WMO, mkondo joto huko Ulaya unafuatia ule mwaka huu huko Australia, India, Pakistani na baadhi ya  maeneo ya Mashariki ya Kati na kwamba mwenendo wa joto unatabiriwa zaidi kwenye maeneo ya kaskazini mwa Ikweta msimu huu wa joto.

Kila mwaka, joto kupita kiasi husababisha vifo vya maelfu ya watu na pia ni chanzo cha mioto ya nyika na kuharibika kwa mifumo ya umeme ya kitaifa.

Kati ya mwaka 2000 na 2016 watu waliokumbwa na mikondo jote kote duniani walifikia milioni 126.