Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani vikali shambulio la bomu Kabul

Picha ya maktaba ikionesha familia ikimbia kupitia barabra iliyojaa vumbi Afganistan
UNAMA/Fraidoon Poya
Picha ya maktaba ikionesha familia ikimbia kupitia barabra iliyojaa vumbi Afganistan

UN yalaani vikali shambulio la bomu Kabul

Amani na Usalama

Watoto kadhaa ni miongoni mwa waliojeruhiwa katika shambulio la bomu kwenye jengo la serikali hii leo mjini Kabul nchini Afghanistan ambalo limetokea karibu na shule kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF.

Henrietta Fore mkurugenzi mtendaji wa UNICEF akilielezea shambulio hilo amesema ni la kusikitisha na kutisha na kwamba “Bomu hilo lililokatili maisha ya watu halikuwanusuru watoto katika muda wa harakati nyingi mjini Kabul watoto ambao walikuwa katika harakati zao muhimu za kila siku za shule”

Kwa mujibu wa duru mbalimbali watu watatu wameuawa na zaidi ya 90 kujeruhiwa wakati bomu kubwa lililokuwa kwenye gari lilipolipuliwa na wanamgambo ambao kisha walivamia jengo la serikali na kuanza mapambano ya risasi yaliyodumu kwa saa saba.

Bi. Fore ameongeza kwamba “shule zinapaswa kuwa mbingu ya amani na machafuko ndani na kuzunguka maeneo ya shule ni jambo lisilokubalika asilani . Hali ya Afghanistan ambayo ni mbaya sasa imezidi kuzorota na machafuko haya ambayo yanakatili maisha na mustakabali wa vijana ni lazima yakomeshwe.”

UNICEF imerejelea wito wake kwa pande zote katika mzozo wa Afghanistan kukomesha mzunguko wa machafuko na kuwalinda watoto wakati wote. Vizazi vya watoto wa Afghanistan imesema hakuna wanalolijua Zaidi ya vita”Na wakati umewadia sasa watoto hawa wafurahie Maisha bila machafuko na vita”.

Nao mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan UNAMA umetoa tamko ukisema Umoja wa Mataifa umechukizwa na shambulio hilo na kutaka kukomeshwa kwa mashambulizi katika maeneo ya raia.

Shambulio hilo limekuja siku chache tu baada ya UNICEF kusema kwamba watoto katika maeneo ya vita ikiwemo Afghanistan wananyimwa mahala salama pa kusoma wakati wa kuchagiza kampeni ya azimio la kutaka shule salama, ambalo ni la kulinda wanafunzi , walimu, shule na vyuo vikuu wakati wa vita na kuruhusu vijana kuendelea na elimu.