Ulinzi zaidi wahitajika kwa wakimbizi ambao ni LGBTI:OHCHR/UNHCR

1 Julai 2019

Nchi na wadau wengine wanaohusika na masuala ya ulinzi kwa wakimbizi wametakiwa kutambua mahitaji maalum na hali tete inayowakabili wakimbizi na wanaoomba hifadhi ambao ni wasagaji, mashoga, wanaofanya mapenzi ya jinsia zote na waliobadili jinsia LGBTI.

Wito huo umetolewa leo kwa pamoja na mtaalam huru wa Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi dhidi ya ukatili na ubaguzi utokanao na mwelekeo wa kimapenzi na jinsia, Victor Madrigal-Borloz na kamishina mkuu msaidizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi kwa ajili ya masuala ya ulinzi Volker Turk.

Mtaalam huyo huru amesema “kwa watu wengi wa jamii ya LGBTI, madhila na unyanyasaji vinaanza mapema hata kabla ya kupanda ndege kukimbilia kwenue usalama. Ubaguzi na mateso mara nyingi vinafanyika kupitia sharia ambazo zinaharamisha mtazamo wao wa kimapenzi, jinsia au mwelekeo wao haliI ambayo ni ubaguzi.”

Ameongeza kuwa watu wa LGBTI pia wanakabiliwa na kuwekwa rumande mara kwa mara , ukatili toka kwa polisi, ghasia na mauaji ambayo hufanywa na serikali na wadau ambao sio wa serikali, lakini pia unyanyasaji katika mazingira ya tiba ikiwemo kushinikizwa kuwa mgumba na kile kinachoitwa huduma kwa kujibadilisha.Kana kwamba hii haitoshi haki zao za kujieleza, kukusanyika na kujumuika pia zinawekewa vikwazo.

Kwa upande wake kamshina msaidizi wa masuala ya ulinzi wa UNHCR bwana Turk amesema “kwa bahati mbaya safari ya kuelekea kwenye usalama inaweza kuwa ya changmoto kubwa kwa wakimbizi wa jamii ya LGBTI ambao wanaendelea kukabiliwa na ubaguzi na ukatili katika nchi wanazopitia kwa muda nan chi zinazowahifadhi.”

Kwa pamoja viongozi hao wanasema kipengee cha kwanza cha ulinzi ni fursa ya kupata hifadhi “na ni muhimu kwa nchi kuhakikisha kwamba hofu itokanayo na mateso kwa sababu ya misingi ya mwekeleo wa kimapenzi, jinsia zao, mtazamo wao wa kingono vinakubalika kama msingi kwa kutambua hali ya ukimbizi. Hivi sasa nchi 37 zinatoa hadhi ya hifadhi kwa watu katika msingi hiyo lakini asilimia kubwa ya nchi ambazo zinatoa hifadhi zimeshindwa kuzingatia misingi hiyo.”

Wamependezeka kuwa maafisa wanaohusika na mchakato wa kubaini hali ya wakimbizi na kudhibiti vituo vya mapokezi ni lazima wapatiwe mafunzo muafanya kuhusu mwelekeo wa kimapenzi, jinsia, na hulka za kimapenzi, na mafunzo haya yatajumuisha tathimini ya mtu binafsi ya mahitaji ya ulinzi kwa wakimbizi na waomba hifadhi toka jamii ya LGBTI. Mbinu mufaka za kutumia kubaini hayo wamesema ni pamoja na kuwahoji na kutumia mbinu zingine za kufanya tathimini ambazo zitaheshimu utu na faragha zao.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud