Uhamisho ni muhimu kwa maisha ya wakimbizi na unahitaji kuimarishwa-UNHCR

1 Julai 2019

Kwa mujibu wa makadirio mapya yaliyozinduliwa hii leo Julai Mosi mjini Geneva Uswisi, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema zaidi ya wakimbizi milioni 1.44 ambao kwa sasa wanaishi katika nchi 60 watahitaji kuhamishwa ifikapo mwaka 2020.

Kamishina Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi akifungua mkutano wa mwaka wa pande tatu kuhusu mashauriano na uhamiashaji wakimbizi ATCR amesema, “kutokana na idadi ya watu wanaohitaji usalama kwa sababu ya vita, migogoro na mateso pamoja na ukosefu wa suluhu za kisiasa za hali hizo, tunahitaji haraka nchi kujitokeza na kuwahamisha wakimbizi.”

Ripoti hiyo ya makadirio ya mahitaji ya uhamisho wa wakimbizi kidunia kwa mwaka 2020 iliyoizinduliwa katika mkutano huo wa ATCR, wakimbizi walioko hatarini zaidi na wanaohitaji kuhamishwa ni pamoja na wakimbizi wa Syria asilimia 40, wakifuatiwa na wale wa Sudan Kusini asilimia 14 na wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo asilimia 11.

“Asilimia 80 ya wakimbizi wote duniani wakiwa katika nchi zinazoendelea nazo zikiwa zinakabiliana na changamoto zake za maendeleo na uchumi na ambao watu wao wanaweza kuwa wanaishi chini ya mstari wa umaskini, kunahitajika kuwepo kugawana majukumu kwa janga hili la dunia. Historia imeonesha kuwa mataifa yanaweza kuungana na kuwasaidia mamilioni ya watu kufika kwenye usalama, kupata makazi na kujenga mstakabali katika jamii mpya.” Amesema Grandi.

Kikanda, kanda ya mashariki na pembe ya Afrika ina mahitaji makubwa zaidi ya wanaohitaji kuhamishwa wakifikia 450,000, ikifuatiwa na Uturuki 420,000 ambayo inahifadhi wakimbizi milioni 3.7, mashariki ya kati na ukanda wa kaskazini mwa Afrika 250,000, Afrika ya kati na maziwa makuu takribani wakimbizi 165,000.

Mwaka uliopita yaani 2018, nchi 25 ziliwachukua wakimbizi 92,400 kwa ajili ya kuwapatia makazi, 55,680 wakiwa kupitia mpango wa UNHCR wa kuwatafutia wakimbizi nchi ya tatu.

 

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter