Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunakusudia kuyapandisha malengo ya maendeleo endelevu kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro-Munyaradzi Muzenda

Wachechemuzi wa malengo endelevu, SDGs yaliyopitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa 2015
UN SDGs
Wachechemuzi wa malengo endelevu, SDGs yaliyopitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa 2015

Tunakusudia kuyapandisha malengo ya maendeleo endelevu kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro-Munyaradzi Muzenda

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa imesalia miaka 11 kuelekea mwaka 2030 ambao ndiyo umepangwa na Umoja wa Mataifa kuwa mwaka ambao malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yatakuwa yametimizwa, Umoja wa Mataifa na wadau mbalimbali wameendelea kuhamasisha umma kwanza kuyafahamu malengo yenyewe na pia kuyatekeleza. Miongoni mwa wadau hao ni Munyaradzi Muzenda kutoka Zimbabwe ambaye ni mkurugenzi wa taasisi ya Africa Speaks, yeye anaendesha kampeni ya kukuza uelewa kuhusu SDGs, Arnold Kayanda na maelezo zaidi.

Akiwa nchini Tanzania katika harakati za kuwahamasisha vijana na wadau wengine kushiriki katika kufanikisha SDGs, Bwana Muzenda kupitia mahojiano na Stella Vuzo wa wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa UNIC Dar es Salaam ameeleza juu ya mpango wao wa kuyapandisha malengo hayo 17 juu ya mlima mrefu zaidi barani Afrika, Kilimanjaro kama moja ya kuyatangaza malengo kwa ulimwengu.

Sauti ya Munyaradzi Muzenda

“Ajenda sasa ni kuwahamasisha wadau kuungana na kutusaidia kupanda Mlima Kilimanjaro. Na kwa kuwa Umoja wa Mataifa wanahamasisha malengo 17 ya SDGs, ambayo yanafahamika kama Ajenda 2030 sasa tunataka kutafuta mtu mmoja mmoja kutoka nchi 17, mwanaharakati ambaye anahusika na lengo fulani kati ya malengo hayo ambapo kwa maana hiyo nchi 17 zitapandisha malengo 17 katika kilele cha mlima Kilimanjaro.”

Bwana Muzenda anasema mawazo haya ndiyo aliwaeleza viongozi wa Muungano wa Afrika mjini Addis Ababa Ethiopia kuwa Afrika wanayoitaka hususani vijana, iko katika malengo hayo yanayotakiwa kuwa yamefikiwa ifikapo mwaka 2030.

Sauti ya Munyaradzi Muzenda

“Kwetu sisi Malengo ya maendeleo endelevu,SDGs ndiyo matumaini yetu, na Afrika tunayoitaka imo katika malengo hay. Ndiyo maana tunataka kufanya hivyo, na Tanzania itakuwa nchi ya kwanza kuyapandisha malengo hayo katika kilele cha mlima Kilimanjaro.”

 SDGs, Mlima Kilimanjaro, UNIC Dar es Salaam, Munyaradzi Muzenda, Africa Speaks