Miongoni mwa tulizokuwa nazo wiki hii

29 Juni 2019

Mtoto mmoja mhamiaji hufariki dunia au kupotea kila siku, UN yataka ulinzi zaidi. Chonde chonde wasafiri pateni chanjo dhidi ya Surua imesisitiza WHO. Kuongeza ushindani wa SMEs ni muarobaini wa kufanikisha SDGs imeeleza Ripoti. Ripoti nyingine imesema familia nyingi za mzazi mmoja duniani zinaongozwa na wanawake. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limeteua muimbaji nyota wa nyimbo za injili Mercy Masika kuwa balozi.

Nitatumia kipaji na upendo wangu kuwakirimu wakimbizi: Mercy Masika balozi mwema wa UNHCR

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limeteua balozi mpya kutoka nchini Kenya, si mwingine bali ni muimbaji nyota wa nyimbo za injili na mwenye hamasa ya kusaidia jamii, Mercy Masika ambaye anasema atatumia kipaji chake kukirimu wakimbizi.

Kwa takriban miaka miwili Mercy amekuwa akisaidia kampeni ya UNHCR inayotoa changamoto ya kuelewa kuhusu ukimbizi Afrika ijulikanayo kama UNHCR’s LuQuLuQu campaign. Kuhusu uteuzi wake Mercy anasema “ni heshima kubwa na furaha kupewa fursa hii. Wakimbizi ni watu kama wewe na mimi na wanaweza kuwa yeyoyote kati yetu, naamimi kama jamii ya Kiafrika tuna jukumu la kuonyesha utu wa kubebeana mizigo kwa kudhihirisha wema wetu kwa matatizo ya wakimbizi.”

 

Familia nyingi za mzazi mmoja duniani zinaongozwa na wanawake- Ripoti

Umri wa mwanamke kuolewa umeongezeka duniani kote na viwango vya uzazi vimeshuka huku wanawake wakizidi kuwa na nguvu kiuchumi, imesema ripoti mpya iliyotolewa wiki hii na Umoja wa Mataifa kuhusu mienendo ya maendeleo ya wanawake duniani bila kusahau familia.

Ikipatiwa jina, “Maendeleo ya Wanawake 2019-2020: Familia katika ulimwengu unaobadilika,” ripoti hiyo iliyoandaliwa na shirika linaloshughulikia masuala ya wanawake la Umoja wa Mataifa, UN-Women imesema kuwa kwa ujumla, theluthi moja ya kaya ni za wanandoa wanaoishi na familia, huku familia zinazojumuisha ndugu na jamaa ni asilimia 27 huku idadi kubwa ya asilimia 8 ya kaya za mzazi mmoja zikiwa zinaongozwana wanawake.

 

Kuongeza ushindani wa SMEs ni muarobaini wa kufanikisha SDGs- Ripoti

Umoja wa Mataifa umetaka uwekezaji zaidi kwenye biashara ndogo na za kati, SMEs kwa kuwa ndio msingi wa kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Kituo cha biashara cha kimataifa, ITC ambayo ni ofisi tanzu ya kamati  ya biashara na maendeleo ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD, imesema hayo kupitia ripoti yake mpya iliyotolewa wiki hii ikisema kuwa msisitizo ni biashara ndogo na za kati kwa kuzingatia mambo makuu manne.

 

 

Chonde chonde wasafiri pateni chanjo dhidi ya Surua- WHO

Kufuatia ongezeko la hivi karibuni la visa vya ugonjwa wa surua katika maeneo mbalimbali duniani hata katika nchi zilizoendelea, shirika la afya ulimwenguni WHO limetoa angalizo hususan kwa wasafiri kupata upya chanjo dhidi ya ugonjwa huo iwapo hawana uhakika kama waliwahi kupatiwa au la.

WHO imetoa angalizo hilo leo kupitia taarifa iliyotolewa mjini Geneva, Uswisi ikisema kuwa hivi sasa ugonjwa huo umesambaa kwa kasi kwa watu ambao bado hawajapatiwa chanjo hiyo.

Shirika hilo limesema kwa watoto wadogo ambao hawajachanjwa dhidi ya Surua, wako hatarini zaidi kuambukizwa na kwamba mtu mwenye kinga ndogo hususan ambaye hakupatiwa chanjo mbili  dhidi ya Surua anaweza kuambukizwa.

 

Mtoto mmoja mhamiaji hufariki dunia au kupotea kila siku, UN yataka ulinzi zaidi

Takribani watoto 1,600 waliripotiwa kufariki dunia au kupotea kati ya mwaka 2014 hadi 2018, imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Ijumaa ya wiki hii, ikimanisha kuwa kwa wastani, mtoto mmoja alitoweka kila siku.

Ikiwa imetolewa na kitengo cha uchambuzi wa data duniani, GMDAC, cha shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, ripoti hiyo yenye jina, “Safari Hatari” inamulika umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi zaidi za vifo na kupotea kwa wahamiaji  hususan watoto, ambao ndio kundi lililo hatarini zaidi.

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud