Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtoto mmoja mhamiaji hufariki dunia au kupotea kila siku, UN yataka ulinzi zaidi

Takwimu zinaonesha tangu mwaka 2014, kuwa takribani watoto 1,600 wamefariki dunia ulimwenguni kote wakisaka maisha bora.
IOM
Takwimu zinaonesha tangu mwaka 2014, kuwa takribani watoto 1,600 wamefariki dunia ulimwenguni kote wakisaka maisha bora.

Mtoto mmoja mhamiaji hufariki dunia au kupotea kila siku, UN yataka ulinzi zaidi

Wahamiaji na Wakimbizi

Takribani watoto 1,600 waliripotiwa kufariki dunia au kupotea kati yam waka 2014 hadi 2018,  imesema ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo, ikimanisha kuwa kwa wastani, mtoto mmoja alitoweka kila siku.

Ikiwa imetolewa na kitengo cha uchambuzi wa data duniani, GMDAC, cha shirika la  uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF, ripoti hiyo yenye jina, “Safari Hatari” inamulika umuhimu wa kuwa na takwimu sahihi zaidi za vifo na kupotea kwa wahamiaji  hususan watoto, ambao ndio kundi lililo hatarini zaidi.

 “Ukosefu wa takwimu kwa msingi wa umri, tabia na hali ya hatari kuhusu wahamiaji watoto waliopotea kunaweka pengo kubwa katika mikakati ya kuwalinda,” amesema Frank Laczko, Mkurugenzi wa Kituo hicho cha uchambuzi wa data.

Amesema hali hiyo inasababishwa mkwamo katika kuandaa mipango na sera za kulinda watoto.

Theluhi mbili ya wanaozama Mediteranea bado hawajulikani walipo

Ripoti hiyo imeangazia wahamiaji waliotoweka kwenye bahari ya Mediteranea na kueleza kuwa katika kipindi hicho cha kuanzia 2014 hadi 2018, IOM iliripoti vifo vya wahamiaji 32,000.

Zaidi ya nusu yao, sawa na 17,900, walikufa maji kwenye bahari ya Mediteranea au walipotea, na kwamba mabaki ya miili yaw engine theluthi mbili bado hayajapatikana.

Kuhusu warohingya wanaokimbia mateso na mzozo nchini mwao Myanmar, ripoto inasema kuwa wao ndio idadi kubwa ya waliokufa kwa mujibu wa ripoti ya vifo wakati wa misafara ya wahamiaji huko kusini-mashariki mwa Asia kati ya 2014-2018.

Katika kipindi hicho wahamiaji 2,200 walipoteza maisha ambapo 1,723 ni warohingya.

Watoto ni miongoni mwa wahamiaji kutoka Amerika ya Kati ambao wanatembea kuelekea Marekani. Pichani ni mmoja wa watoto waliokuwa wamepigwa picha kwenye mitaa ya Tapachula, Chiapas nchini Mexico tarehe 21 Oktoba 2018
UNICEF México
Watoto ni miongoni mwa wahamiaji kutoka Amerika ya Kati ambao wanatembea kuelekea Marekani. Pichani ni mmoja wa watoto waliokuwa wamepigwa picha kwenye mitaa ya Tapachula, Chiapas nchini Mexico tarehe 21 Oktoba 2018

Na kuhusu misafara ya wahamiaji kutoka Mexico kwenda Marekani, katika kipindi husika, idadi ya vifo imekuwa ikiongezeka na k ufikia 1,907.

Ripoti hiyo imechapishwa siku chache baada ya picha ya kusikitisha na kushtusha ya mtoto na baba  yake waliokufa maji kando mwa mto unaotenganisha Marekani na Mexico.

Ni kutokana na picha hiyo, mkuu wa UNICEF alitoa wito kwa nchi zichukue hatua zaidi kulinda wahamiaji walio hatarini.

Uchambuzi wa kina wa takwimu kuhusu wahamiaji zinapatikana kwenye wavuti mradi wa IOM kuhusu wahamiaji waliopotea.

Hatua ya IOM kujikita katika watoto wahamiaji ni sehemu ya mpango mpana wa kutaka takwimu zaidi za kundi hilo, mpango ambao unahusisha UNICEF na mashirika mengin ikiwemo lile la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo, OECD.