Wahamiaji wana haki na wanasitahili usaidizi-Nick Ogutu

28 Juni 2019

Mkutano wa 16 wa kuhusu haki za binadamu, uhamiaji na vijana leo umeingia siku yake ya pili katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. Mkutano huo wa kimataifa unaofanyika kila mwaka unawakutanisha wadau wa haki za binadamu kutoka kote duniani na mmoja wa waliohudhuria ni rais wa taasisi inayoitwa ‘Safari yangu’, inayosimamiwa na Chuo Kikuu cha Columbia cha hapa Marekani, Bwana Nick Ogutu.

Katika mahojiano nami, Bwana Ogutu ameanza kwa kunieleza kile wanachokifanya katika taasisi ya ‘Safari yangu’.

“Safari yangu, kazi tunayoifanya ni kuangalia mambo ya haki ya wale waliotoka kwao sanasana Afrika. Katika wahamiaji kuna wale walio na vibali na wale ambao hawana. Lakini kibinadamu wote ni sawa wana haki na wote tunawatetea. Hata wale walio na makaratasi kuna shida walizonazo, kifamilia, kibiashara na maisha yao. Lazima tuwatetee.”

Kiongozi huyo wa taasisi ya ‘Safari yangu’ akitoa mfano wa moja ya mafanikio waliyoyafikia, amesema ni jinsi  walivyowasaidia wafanyabiashara ndogondogo(wamachinga) waliokuwa wakipanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara huku wakiathirika na hali ya hewa mathalani wakati wa baridi kali.

“Ilituchukua kama miezi mitano tukietembea tukitafuta lakini mwishowe tukapata jengo fulani, hao watu wakakubali kutupatia nafasi. Wale watu waliokuwa wanauza kandoni mwa barabara sasa wamepata nafasi ya kuuza ndani iwe ni msumu wa baridi au joto wanaweza kuuza na biashara inaendelea.”

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud