Dunia inatazama kinachoendelea Idlib; tushikamane na wananchi- Kampeni

27 Juni 2019

Viongozi 11 wa mashirika ya misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa na wadau wao wamezindua kampeni ya kimataifa ya kuonesha mshikamano na wananchi wa kaskazini-magharibi mwa Syria ambao hivi sasa wanakabiliwa na mashambulizi makubwa ya kijeshi.

Taarifa iliyotolewa leo mjini New York, Marekani na Geneva, Uswisi na viongozi hao imesema kuwa kampeni hiyo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa, “raia milioni 3, miongoni mwao watoto milioni 1 wanakabiliwa na tishio la mapigano yanayoendelea kwenye jimbo la Idlib na viunga vyake.”

Kampeni inasema, Tunawaona, Tuko nanyi, Hamjasahaulika, Ninyi si Walengwa na #Duniainatazama.

Ujumbe mahsusi kwa wasyria

Katika ujumbe wao wa video, viongozi hao wamesisitiza kuwa, “raia wanakumbwa na tishio la ghasia na mapigano na wanahaha kupata ulinzi. Wengi wameshauawa na hata vita ina sheria. Tunachukizwa na madhara makubwa yanayoendelea ya mashambulizi hayo kwa hospitali, shule na masoko.”
 
Viongozi hao wameonya kuwa “Idlib iko  hatarini kuwa jinamizi la kibinadamu kuliko kitu chochote kile ambacho kimewahi kushuhudiwa karne hii.”

© UNICEF/Khalil Ashawi
Hospitali ya upasuaji ya Kafr Nubl ikiwa imesambaratishwa kufuatia mashambulizi ya mwezi Mei 2019. Jengo na gari la wagonjwa vyaonekana kwenye kifusi.

Miongoni mwa viongozi hao ni Mark Lowcock, mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya dharura, OCHA ambaye amesema, “hofu yetu kubwa zaidi sasa imefika na bado raia wasio na hatia wanaendelea kulipa gharama za kushindwa kwa utashi wa kisiasa wa kusitisha ghasia na kufanya kile kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa; kulinda rais.”

Amesema kwa wanawake, watoto na wanaume wa Idlib, kinachofanyka sasa ni adhabu ya kifo na kwamba, “kampeni yetu ya inaonesha mshikamano na familia zilizo chini ya mashambulizi na kumweleza kila mtu kuwa tunatazama na kushuhudia kinachoendelea.”
 

Wananchi wakimbizi Syria

Idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani kutoka maeneo mengine ya Syria imeongezeka maradufu tangu mwaka 2015 kuzidi idadi ya wakazi wa Idlib. 
Takribani watu 330,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani kwenye eneo hilo katika miezi miwili ya ongezeko la mapigano.

Umoja wa Mataifa unasema kuwa watu hawana pa kukimbilia na Katibu Mkuu wa umoja huo Antonio Guterres ameonya kuhusu mapigano hayo kwa miezi kadhaa sasa lakini hayajakoma au hata kupungua.

© UNICEF/Aaref Watad
Familia 400 zimepata hifadhi katika kituo cha makazi ya muda huko Idlib nchini Syria na watoto nao wamepata fursa ya kusomea kwenye mahema

Mashirika husika kwenye kampeni

Kampeni hii inaenda sambamba na kuchapishwa kwa video ya kampeni kwenye mtandao wa Twitter na majukwaa mengine ya mitandao ya kijamii ambapo viongozi wa dunia na wananchi wanashawishiwa kuisambaza katika mitandao yao kuonesha mshikamano na kusisitiza kuwa wanaona kinachoendelea Idlib.

Viongozi wahusika kwenye kampeni hii wanatoka mashirika ambayo ni UNICEF, OCHA, Save The Children, Baraza la wakimbizi la Norway, Oxfam America, World Vision, UN Women, CARE International, Kamati ya uokozi ya kimataifa, Mercy Corps, IOM, Concern Worldwide na WFP.

Twatumai G-20 itamulika hali ya Syria- Pedersen

Wakati kampeni hiyo inazinduliwa, Baraza la Usalama nalo lilikuwa na kikao  kuhusu hali ya kisiasa nchini Syria, ambapo mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa taifa hilo, Geir Pedersen, amesema hali bado inatisha, mashambulizi ya angani na makombora kila uchao huku kikundi cha cha Hayat Tahrir al-Sham kilichotangazwa na baraza hilo kuwa ni cha kigaidi, kikiendeleza mashambulizi huko Idlib.

Amesema mashambulizi hayo lazima yakome huku akiongeza kuwa kwa hali ya sasa ilivyo hakuna kundi lililo hai la kimataifa ambalo usaidizi wake una hakikisho la kuleta pamoja pande kinzani.

“Natumai, hatua zangu zinaweza kusaidia kuleta pamoja wahuka kwa mfumo wa Asana. Na ndio  maana naendelea kukaribisha watu muhimu zaidi kwenye mkutano wa pamoja kusaidia mchakato wa amani utakaoongozwa na wasyria wenyewe,” amesema Bwana Pedersen.

Ameongeza kuwa ni matumaini yake kuwa mkutano wa kundi la mataifa 20, G20 unaofanyika kesho huko Tokyo, Japan utaweza kujumuisha ajenda ya Syria.

“Mimi na Katibu Mkuu tumesihi Syria iwe moja ya ajenda muhimu. Tunatumai Urusi na Uturuki zinaweza kushirikiana katika ngazi ya juu kuleta utulivu Idlib,” amesema mjumbe huyo maalum.

Halikadhalika amesema wanatumai kuwa Urusi na Marekani zinaweza kujenga msingi kutokana na mazungumzo ya hivi karibuni na kuwa na mazungumzo ya dhati zaidi, “kwa sababu ushirikiano kati yao ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa juu ya Syria.

 

Je Vipaumbele ni vipi?

Wakati huo huo, Najat Rochdi, ambaye ni mshauri mwandamizi wa kibinadamu kwa mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Syria, ametoa taarifa yake akitaka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa waunge mkono haraka vipaumbele vya taifa hilo la Mashariki ya Kati,
 
Vipaumbele hivyo ni pamoja na kusitisha kwa mapigano huko Idlib, ili kulinda raia.

Halikadhalika Bi. Rochdi ametaja kipaumbele cha pili kuwa ni huko Rukban ambako watu 27,000 hawana huduma za msingi na wanahitaji pia huduma za ulinzi. “Umoja wa Mataifa unataka uhakika wa kufikisha misaada ya kibinadamu,” amesema mshauri huyo akiongeza kuwa, “msaada wamepatiwa watu 14,800 waliokimbia makazi ya muda.”

Ametaja kipaumbele cha tatu kuwa ni kwa watu 73,000 ambao bado wamesalia kambi ya Al Hol wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wachanga.

Kipaumbele cha nne ni kukamilisha ombi la usaidizi kwa Syria la dola bilioni 3.3 kwa ajili ya kusaidia wasyria milioni 11 kwa mwaka huu wa 2019 akisema  hadi sasa ombi hilo limechangiwa kwa asilimia 23 pekee.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter