Skip to main content

Sasa mwelekeo ni sahihi kutokomeza ugonjwa wa vikope mwaka 2020

Msambazaji dawa kwenye jamii akiwa na kasha lake la dawa dhidi ya upofu kuelekea kijiji cha ndani zaidi huko Cameroon
WHO
Msambazaji dawa kwenye jamii akiwa na kasha lake la dawa dhidi ya upofu kuelekea kijiji cha ndani zaidi huko Cameroon

Sasa mwelekeo ni sahihi kutokomeza ugonjwa wa vikope mwaka 2020

Afya

Idadi ya watu walioko hatarini kuugua ugonjwa wa vikope, ugonjwa ambukizi unaoongoza duniani kwa kusababisha upofu imepungua kwa asilimia 91, limesema shirika la afya ulimwenguni, WHO.
 

Hii inamaanisha kuwa maambukizi yamepungua kutoka watu bilioni 1.5 mwaka 2002 hadi watu zaidi ya milioni 142 mwaka huu wa 2019.

Takwimu mpya zilizowasilishwa mjini Geneva, Uswisi kwenye mkutano wa 22 wa ubia wa WHO wa kutokomeza ugonjwa wa vikope ifikapo mwaka 2020, GET2020 zimeonesha pia kuwa “idadi ya watu wanaohitaji upasuaji kwa ajili ya kutibu hatua ya mwisho kabisa ya ugonjwa huo ambayo inaweza kusababisha upofu, imepungua kutoka watu milioni 7.6 mwaka 2002 hadi watu milioni 2.5 mwaka 2019, sawa na asilimia 68.”

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa WHO anayehusika na magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika, NTDs Dokta Mwele Malecela amesema,  “kutokomeza ugonjwa wa vikope kunachangia afya ya jicho na uoni na ubora wa maisha kwa watu walio maskini zaidi, watu walio pembezoni zaidi na hivyo kukaribia zaidi kufikia ahadi ya huduma ya afya kwa wote.”

Dkt. Mwele amesema kuondokana na ugonjwa wa vikope, kumefanikiwa kutokana na ukarimu na mchango wa dawa ya azithromycin, na michango endelevu kutoka kwa wahisani sambamba na juhudi za wafanyakazi walio mstari wa mbele kutoa huduma na tiba kwa jamii.

Mkakati wa SAFE

Hata hivyo ugonjwa wa vikope umesalia tatizo kwa mataifa 44 na umesababisha upofu au uoni hafifu kwa watu  milioni 1.9 duniani kote, imesema WHO.

Ugonjwa wa vikope husababishwa na vimelea au bakteria ambapo ufuatiliaji na tiba yake umekamilishwa kupitia mbinu za utambuzi wa maeneo uliopo, hatua za kudhibti kwa mkakati wa SAFE ambao ni upasuaji, tiba, usafishaji wa uso na uboreshaji usafi wa mazingira.

Tangu mwaka 2011, mataifa 8 yamethibitishwa na WHO kuwa yametokomeza ugonjwa wa vikope kama tatizo la afya ya umma. 

Halikadhalika WHO inasema nchi moja ambayo awali ugonjwa wa vikope ulikuwa tishio la afya kwa umma sasa imesonga mbele kwa kudhihirisha ufanisi wa mpango wa SAFE.

GET2020

Mkakati wa GET2020 ulianzishwa mwaka 1996 na WHO kwa kushirikiana na wadau wake ili kutekeleza mpango wa SAFE.

WHO inasema kazi ya kutokomeza ugonjwa wa vikope si aghali, ni rahisi na ina manufaa na huleta faida kubwa ya kiuchumi.