Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda kidedea tuzo za FAO; ni kwa mchango wake wa kuinua vijana vijijini

Utangamano mzuri na wakimbizi husababisha uchumi kuchanua nchini Rwanda
UNHCr/Anthony Karumba
Utangamano mzuri na wakimbizi husababisha uchumi kuchanua nchini Rwanda

Rwanda kidedea tuzo za FAO; ni kwa mchango wake wa kuinua vijana vijijini

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Serikali ya Rwanda na kundi la waandishi wa habari kutoka Hispania ni miongoni mwa washindi wa tuzo mbalimbali za shirika la chakula na kilimo duniani, FAO kuhusu sekta ya kilimo ulimwenguni.

Tuzo hizo zimetolewa mjini Roma, Italia ambapo Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva amepongeza washindi wote akisema, “asanteni kwa mchango wenu na ni muhimu sana kuonyesha matokeo chanya na njia thabiti ambazo kwazo tunaweza kufanya kazi pamoja.”

Mathalani Wizara ya Kilimo ya Rwanda, “ilitambuliwa kwa mbinu yake ya kipekee ya kushughulikia ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana maeneo ya vijijini.”

Mbinu yao ilihusisha pamoja na mambo mengine ushirikiano na chama cha vijana kwenye sekta ya kilimo na biashara nchini humo, RYAF pamoja na serikali za mitaa na taasisi binafsi kuchagiza fursa za ajira kwa vijana maeneo ya vijijini.

Nao wahariri wa gazei la El Pais kutoka Hispania wao waliibuka kidedea na kushinda tuzo ya  A.H. Boerma kwa mchango wao wa kipekee wa kuhabarisha umma kuhusu ajenda 2030 au malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ambapo taarifa ya FAO imesema kuwa “wakijikita zaidi kwenye njaa, utapiamlo, kilimo endelevu na dhima ya FAO katika kuimarisha upatikanaji wa chakula na lishe.”

Wizara ya Kilimo nchini Pakistani, nayo ilitambuliwa kwenye tuzo hizo kwa jitihada zake za kipekee za kutekeleza mradi wa kutokomeza ugonjwa wa miguu na midomo kwa wanyama, FMD, mradi ambao ulichochea kampeni kubwa ya chanjo na kujenga uwezo wa mtandao wa maabara nchini kote.

Wafanyakazi wawili wa ughani wa FAO nao  wanaofanya kazi nchini Sudan Kusini na Yemen nao waliibuka na tuzo ya B.R. Sen Award inayotambua wafanyakazi wa mashinani wa shirika hilo wanaosongesha miradi ya kitaifa kule waliko.

Miongoni mwao ni Serge Tissot ambaye ametambuliwa kwa uongozi wake wa kipekee na utaalamu wa kiufundi akiwa mwakilishi wa FAO huko Sudan Kusini ilhali Salah El Hajj Hassan ameshinda tuzo kwa mchango wake wa kipekee katika kushughulikia tatizo la uhakika wa chakula, maendeleo ya vijijini na changamoto za kibinadamu akiwa mwakilishi wa FAO nchini Yemen.

Washindi wengine ni meli ya utafiti kutoka Norway na wabunge wa sasa na wastaafu nchini Chile.

TAGS: FAO, Tuzo, Rwanda, Pakistani, Chile