Kila tunakokimbilia na wanangu, ni kaburi-Mkimbizi Yemen

Mfanyakazi wa WFP akiangalia Lori lililoleta msaada wa chakula katika kambi ya Khudais Yemen mwezi Juni 2019
WFP/Mohammed Awadh
Mfanyakazi wa WFP akiangalia Lori lililoleta msaada wa chakula katika kambi ya Khudais Yemen mwezi Juni 2019

Kila tunakokimbilia na wanangu, ni kaburi-Mkimbizi Yemen

Wahamiaji na Wakimbizi

Mwezi huu tarehe 20, shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP Limeanza kwa kiasi kuanza usitishaji wa msaada wa chakula nchini Yemen katika maeneo yaliyokaliwa na mamlaka zenye makao yao mjini Sana’a. Maamuzi hayo yamechukuliwa baada ya majadiliano kuchelewa kuhusu makubaliano ya kuanzisha udhibiti wa kuzuia chakula kuelekezwa kwingine badala ya kwenda kwa walengwa walioko hatarini.

Hatua ya kwanza ya usitishwaji wa msaada wa chakula, kwenye jiji la Sana’a pekee, inawaathiri watu wapatao 850,000. Katika maeneo mengine ya Yemen, msaada wa WFP unaendelea kama kawaida.

Amina na watoto wake saba wameyakimbia makazi yao  kwa miaka minne kutokana na mapigano. Mara ya kwanza alipokimbia, alikuwa anasubiri kupokea chakula wakati wapiganaji walipoingia katika Kijiji chake. Alilazimika kuondoka bila pesa hivyo ili kupata usafiri akalazimika kuwapatia mali zake waliompa usafiri.

(Sauti ya Amina)

“Nimekimbia mara nne katika maisha yangu. Kila wakati ninapofika mahali ni kama kaburi. Kila ninakofika ni kaburi kwangu na wanangu. Ninalia ninapowaona watoto wangu wakiwa na njaa. Ninalia kwasababu siwezi kumudu chakula kwa ajili yao. Ninaweza kupata wapi chakula kwa ajili yao? Wanalala…siwezi kufanya lolote...wakati mwingine ninawapiga walale.”

WFP katika miezi ya hivi karibuni imekuwa ikitoa msaada wa chakula kwa zaidi ya watu milioni 10, hiyo ikiufanya msaada huo kuwa mkubwa kuliko yote inayotekelezwa na shirika hilo kote duniani. WFP inalenga kwa mwezi kuwalisha watu milioni 12 walioko hatarini na wasiokuwa na uhakika wa chakula. Hiyo inafanya lengo la mwaka 2018 kuwa mara mbili. Tobias Flaeming ni afisa wa WFP Yemen anasema,

(Sauti ya Tobias Flaemig wa WFP Yemen)

“Watu wengi katika mji wa Abs wametawanywa siyo mara moja, ni mara mbili, tatu, nne…kila mara wanapotawanywa wanatakiwa kutafuta usafiri, hivyo njia zao za kukabiliana na hali hiyo, kwa kweli kutafuta usafiri, maisha, zinapungua na hivyo kuifanya WFP kuwa muhimu zaidi kuingilia haraka ikiwa na msaada wa haraka kwa siku tano kwa wiki na pia kimsingi kuwafanya watu wabaki hai.”

Katika mwaka huu wa 2019 WFP inalenga kuwasaidia wanawake milioni 3 na watoto na katika kipindi chote cha usitishaji ugawaji wa chakula, itaendelea na programu zake za lishe kwa watoto wenye utapiamlo, wajawazito, wanawake wanaonyonyesha.