Uchunguzi wa kisayansi watumika kubaini washambuliaji Mopti nchini Mali

27 Juni 2019

Nchini Mali, kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya vijiiji na mauaji ya raia katikati mwa nchi hiyo, kitengo cha polisi wanasayansi kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu kwenye taifa hilo la Afrika Magharibi wanafanya uchunguzi wa kina ili kuhakikisha hakuna ukwepaji wa sheria kwa watekelezaji wa mashambulio hayo.

Taswira kutoka angani ya kijiij cha  Hèrèmakono, kwenye jimbo la Mopti, katikati mwa Mali ambalo hivi karibuni lilishambuliwa na watu wenye silaha.

Kionekanacho ni mabaki ya nyumba ya chifu wa kijiji hicho ambayo ilitiwa moto na washambuliaji.

Leo kikundi cha maafisa wa polisi wenye utaalamu wa kisayansi kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu Mali, MINUSMA umewasili ili kuchukua ushahidi kuhakikisha kwamba watekelezaji wanakamatwa na kufikishwa kwenye mkono wa sheria.

Wakiwa na wenyeji wao, polisi hao na vifaa vyao wanakusanya ushahidi na kisha wanarejea kwenye maabara.

 
Geoffrey Chenais ambaye ni polisi mtaalam kwenye kikosi hiki kiitwacho, PTS anasema kuwa maabara yao hufanya kazi kila siku kwa lengo la kusaidia mfumo wa haki nchini Mali kuepukana na ukwepaji sheria na kwamba,

 Sauti ya Geoffrey Chenais

“Halikadhalika tunasaidia kitengo cha haki za binadamu cha MINUSMA katika mashambulizi haya yaliyotokea vijijini hivi karibuni. Lengo in kusaidia kusaka ukweli kwa kukusanya ushahidi ambao hatimaye utawasilishwa kwenye mamlaka za sheria za Mali.”

 
Tangu mwezi Machi mwaka huu hadi mwezi huu wa Juni, kumekuwepo na mfululizo wa  mashambulizi kwenye eneo la kati la Mopti nchini Mali ambayo pamoja na kusababisha vifo vya walinda amani, pia yalisababisha vifo vya raia.

 
 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter