Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madhara yatokanayo na matumizi ya madawa ya kulevya ni kupindukia- UNODC

Mtumiaji wa mihadarati akitumia dawa  mbadala kwa ajili ya kuondowa hamu ya mihadarati
Picha/IRIN/Sean Kimmons
Mtumiaji wa mihadarati akitumia dawa mbadala kwa ajili ya kuondowa hamu ya mihadarati

Madhara yatokanayo na matumizi ya madawa ya kulevya ni kupindukia- UNODC

Afya

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kudhibiti madawa ya kulevya na  uhalifu, UNODC, imesema kuwa madhara ya afya yatokanayo na matumizi ya madawa hayo ni makubwa kuliko ilivyofikiriwa. UNODC imesema hayo wakati wa uzinduzi wa ripoti yake hii leo ikiangazia mwenendo wa matumizi ya madawa ya kulevya duniani mwaka 2017 na madhara yake.

Akiwasilisha ripoti hiyo mbele ya wanahabari mjini New York, Marekani, Miwa Kato ambaye ni Mkurugenzi wa Operesheni wa ofisi hiyo amesema madhara ni makubwa kwa kuzingatia kuwa watu milioni 35 duniani kote wameathirika na wanahitaji huduma za matibabu.

Hata hivyo takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2017 kati ya watu milioni 11 waliojidunga madawa hayo, milioni 1.4 wanaishi na virusi vya ukimwi, VVU, milioni 5.6 wanaugua homa ya ini aina ya C.

UNODC tumebaini takwimu nyingi zaidi kutokana na kuimarika kwa tafiti na takwimu sahihi zaidi, ikiwemo ufahamu zaidi wa kiwango cha matumizi ya madawa kutokana na tafiti mpya zilizofanyika India na Nigeria, mataifa mawili yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani,”amesema Kato.

Ameenda mbali zaidi akisema kuwa, “mwaka  2017, maeneo ya Amerika Kaskazini yameshuhudia ongezeko la idadi ya watu waliofariki dunia kwa kutumia dawa kupita kiasi na kiwango kilikuwa ni ongezeko kwa asilimia 14,” amesema Bi. Kato akiongeza kuwa “nina uhakika sina ulazima wa kuonyesha msisitizo ndani ya hadhira hii kwa kutambua madhara ya tatizo hili kwenye jamii hii.”

Wakati kwa ujumla takwimu za matumizi ya madawa ya kulevya mwaka 2017 zinaonesha kuwa watu waliotumia madawa ya kulevya mwaka jana ni milioni 271, sawa na mwaka uliotangulia, bado mwenendo ni wa kuongezeka kwa kuwa idadi ya watu wanaotumia madawa hivi sasa ni asilimia 30 zaidi ikilinganishwa na miaka 10 iliyopita.

“Ingawa hii ni inachangiwa na ongezeko la idadi ya watu wenye umri wa kati ya miaka 15-64, bado matumizi ya mihadarati Afrika, Asia, Ulaya na Amerika Kaskazini imeongezeka sambamba na matumizi ya bangi huko Amerika ya Kaskazini na Kusini pamoja na Asia,” Amesema Bi. Kato.

Mihadarati ni dawa haramu zinazotolewa kwenye afyuni na kwa mujibu wa Bi. Kato, “kile ambacho kimekuwa kiitwa janga la mihadarani sasa linaathiri Afrika hususan Afrika Magharibi, Kati na Kaskazini. Hii inachangaiwa na Tramadol ambayo imekuwa ikitumiwa kama dawa ya kupunguza maumivu kwa miongo kadhaa na hadi sasa imesalia nje ya udhibiti wa kimataifa.”

UNODC sasa inataka uratibu baina ya taasisi za kitaifa, kikanda na kimataifa ili kuimarisha usimamiaji wa sheria na hatimaye kuvunja mitandao ya biashara za madawa ya kulevya.

Halikadhalika ofisi hiyo imesema hatua za pamoja pia ni muhimu kushughulikia uhusiano kati ya mitandao ya kigaidi na uhalifu na kukabili vikundi vya kigaidi ambavyo vinashiriki, vinanufaika moja kwa moja na shughuli za kihalifu ikiwemo usafirishaji wa madawa ya kulevya.