Hali ya Sudan Kusini bado inahitaji uangalizi wa karibu- Andrew Gilmour

25 Juni 2019

Idadi ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Sudan Kusini imepungua, amesema hii  leo msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  kuhusu masuala ya haki za binadamu Andrew Gilmour.

Akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la umoja huo mjini New York , Marekani,  akiangazia haki  za binadamu nchini humo, Bwana Gilmour amesema taarifa hizo zinatokana na ufuatiliaji uliofanywa tangu mwaka jana na kitengo cha haki za binadamu cha Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS

Amesema kitengo hicho kimeshuhudia kupungua kiujumla kwa idadi ya matukio ya ukiukwaji wa haki za binadamu yaliyokuwa yakifanywa na vikosi vya serikali na makundi yaliyojihami kote Sudan Kusini.

Hata hivyo amesema kumekuwepo na matukio kadhaa ya unyanyasaji wa kingono yanayotekelezwa na pande zote katika mgogoro ambapo idadi kubwa ya matukio hayo ilishuhudiwa mwezi Novemba na Desemba 2018 mjini Bentiu.

Bwana Gilmour anasema, “bado hali ya amani ni tete na inahitaji uangalizi. Katika Equatoria ya kati ambako vikosi vya serikali pamoja na vikundi vya upinzani vimeendelea kupigana na kunaripotiwa, uvunjaji wa haki za binadamu ikiwemo mauaji, utekaji, unyanyasaji wa kingono na kuhamishwa kwa lazima.”

Pichani  ni nchini Sudan Kusini  ambako wafanyakazi wa ofisi ya haki za binadamu  akichunguza ukiukwaji wa haki za binadamu.
UN Photo/JC McIlwaine
Pichani ni nchini Sudan Kusini ambako wafanyakazi wa ofisi ya haki za binadamu akichunguza ukiukwaji wa haki za binadamu.

Ameongeza kuwa katika maeneo mengine ya Sudan Kusini, vurugu zimekuwa zikifanywa na makundi ya kwenye jamii na vurugu hizo zimekuwa pia zikungwa mkono na vikosi vya usalama vya serikali pamoja na makundi mengine.

“Wakati ukiukwaji wa haki za binadamu unaohusishwa na mgogoro vikiendelea, vilevile kuendelea kuwepo kwa vikwazo vya kisiasa kunaendelea kuwa kikwazo. Uhuru wa kujieleza uko katika hali tete, "   ameeleza Bwana Gilmour akiongeza kuwa pia ufuatiliaji wa maisha ya watu, unyanyasaji na ukamatwaji usiofuata sheria umekuwa ukitumika kuzuia shughuli mbalimbali hususani za watetezi wa haki za binadamu, wakosoajina wanahabari.

Katika kuhitimisha, Bwana Gilmour amesema ofisi ya haki za binadamu inapenda kutoa mapendekezo mawili kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mosi,  kuendelea kuzisihi pande zote katika mgogoro wa Sudan Kusini kutekeleza ahadi zao za kumaliza uhasama na kukomesha migogoro.

Pili, kwa jumuiya ya kimataifa kutoa msaada wa  kuweka shinikizo kwa pande zote zinazohusika kuanzisha kwa mipango ya haki iliyotamkwa katika makubaliano ya amani.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter