Familia nyingi za mzazi mmoja duniani zinaongozwa na wanawake- Ripoti

25 Juni 2019

Umri wa mwanamke kuolewa umeongezeka duniani kote na viwango vya uzazi vimeshuka huku wanawake wakizidi kuwa na nguvu kiuchumi,  imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na Umoja wa Mataifa kuhusu mienendo ya maendeleo ya wanawake duniani bila kusahau familia.

Ikipatiwa jina, “Maendeleo ya Wanawake 2019-2020: Familia katika ulimwengu unaobadilika,” ripoti hiyo iliyoandaliwa na shirika linaloshughulikia masuala ya wanawake la Umoja wa Mataifa,  UN-Women imesema kuwa kwa ujumla, theluthi moja ya kaya ni za wanandoa wanaoishi na familia, huku familia zinazojumuisha ndugu na jamaa ni asilimia 27 huku idadi kubwa ya asilimia 8 ya kaya za mzazi mmoja zikiwa zinaongozwana wanawake.

“Familia hizo za mzazi mmoja zinazoongozwa na wanawake ni wale ambao wanahaha huku na kule kubadili kazi moja au nyingine, wakile watoto na kufanya kazi za ndani bila malipo. Familia za wanandoa wa jinsia moja nazo zinaongezeka kwenye kanda zote za dunia,” imesema ripoti hiyo.

Familia pia inaweza kuwa chanzo cha ukatili

Ikichambua familia kama taasisi inayotambuliwa kuwa ni sehemu ya malezi, ripoti hiyo inasema kuwa familia imebainika kuwa inaweza kuwa chanzo cha mizozano, ukosefu wa usawa na ghasia.

“Hii leo, wanawake na wasichana bilioni 3 wanaishi kwenye nchi ambazo ubakaji ndani ya ndoa bado haujaharamishwa wazi,” imesema ripoti hiyo ikiongeza kuwa ukosefu wa wa haki na ukiukwaji mwingine wa haki unafanyika kwa njia nyingine.

Imetolea mfano masuala ya mirathi ambako katika nchi 1 kati ya 5 haki za mirathi kwa wavulana na wasichana ni tofauti, ambapo wavulana wana haki zaidi.

Halikadhalika katika mataifa 19 wanawake wanatakiwa kisheria kuheshimu waume zao, “takribani theluthi moja ya wanawake walioolewa katika nchi zinazoendelea wameripoti kuwa wana sauti ndogo au hawana sauti kabisa juu ya afya zao wenyewe.”

Ripoti ya ILO ya pengo la mishahara 2018/19 imebaini kwamba wanawake bado wanalipwa asilimia 20 pungufu ya wanaume
© ILO/Marcel Crozet
Ripoti ya ILO ya pengo la mishahara 2018/19 imebaini kwamba wanawake bado wanalipwa asilimia 20 pungufu ya wanaume

Fursa za ajira ni finyu kwa wanawake walioolewa

Katika medani za ajira, ripoti inasema kuwa “wanawake wanaendelea kuingia kwenye soko la ajira kwa kiasi kikubwa, “lakini ndoa na uzazi vinakwamisha ushiriki wao wa kina sambamba na kupata kipato sahihi.”

Takwimu zinaonesha kuwa, duniain, zaidi ya nusu ya wanawake walioolewa wenye umri kati ya miaka 25 na 54 wako kwenye soko la ajira ikilinganishwa na theluthi mbili za wanawake ambao hawajaolewa na asilimia 96 ya wanaume waliooa.

Ripoti inasema kuwa kichocheo kikubwa cha ukosefu huo wa usawa ni suala kwamba, “wanawake wanaendelea kufanya zisizo na malipo za malezi mara tatu zaidi na kazi za ndani kuliko wanaume kutokana na kutokuwepo kwa huduma nafuu za uangalizi au malezi.

Hata hivyo ripoti imeangazia maendeleo kwenye likizo za uzazi kwa wanaume hususan katika mataifa ambayo yametenga likizo ya uzazi kwa wanaume.

Kigingi kingine kwa wanawake ni pale ambapo wanataka kuhama ambapo ruhusa inakuwa inatoka kwa mumewe na hivyo kumkwamisha katika harakati iwapo anataka kukimbia ghasia au kusaka ajira bora zaidi.

Nini kifanyike kuwa na mwelekeo bora?

Ili kuondokana na vikwazo vya sasa ripoti ina mapendekezo lukuki kwa watunga sera, wanaharakati na watu wote ili kubadili familia ziwe na msingi wa usawa na haki ambamo kwao mwanamke anaweza kuwa na sauti, chaguo na usalama wa kimwili na kiuchumi.

Miongoni mwao ni kubadilisha na kurekebisha sheria za familia ili kuhakikisha wanawake wanaweza kuchagua aolewe na nani na kwa wakati gani na pia kuweka fursa ya talaka iwapo itahitajika kufanya hivyo.

Pendekezo lingine ni kuwekeza kwenye huduma za umma hususan elimu na afya ya uzazi ili wanawake na wasichana waweze kuwa na fursa ya kuchagua ni lini anataka kuwa na mtoto.

Suala pia la likizo ya uzazi yenye malipo limependekezwa na serikali zisaidia malezi kwa watoto na wazee kama njia mojawapo ya kusaidia familia na kupanua wigo wa fursa kwa wanawake.

Pendekezo lingine ni kuhakikisha kuna sheria zinazotekelezwa za kulinda usalama wa mwanamke dhidi ya aina zote za ukatili na kuwapatia haki na msaada pindi anapokabiliwa na ghasia hizo.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter