Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dagaa na samaki wengine wa dogo wavuliwao mtoni na ziwani ni muarobaini wa njaa na kipato Afrika

Mwanamke nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiwa amebeba dagaa
UN Photo/Abel Kavanagh
Mwanamke nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiwa amebeba dagaa

Dagaa na samaki wengine wa dogo wavuliwao mtoni na ziwani ni muarobaini wa njaa na kipato Afrika

Ukuaji wa Kiuchumi

Shirika la chakula na kilimo duniani, FAO limeibuka na nyaraka yake mpya ambayo inaonesha umuhimu wa samaki wadogo kama vile dagaa katika kufanikisha kutokomeza njaa na kuinua kipato kwa wakazi wa bara la Afrika.

Nyaraka hiyo ya kikazi iliyochapishwa leo inaonesha kuwa dagaa na samaki hao wavuliwao mtoni na ziwani mara nyingi husindikwa, huuzwa na kuliwa wazima wazima n ani robo tatu ya samaki wote wavuliwao kwenye vyanzo hivyo vya maji barani Afrika.

Hata hivyo nyaraka hiyo inasema kuwa licha ya  umuhimu wake kiafya na kuwa na kiwango cha juu cha lishe na na kiwango kikubwa cha uvuvi bado hawapatiwi kipaumbele kutokana na thamani yake ndogo kiuchumi ingawa uvuvi wake hauhitaji teknolojia ya hali ya juu.

FAO imetolea mfano hatua ya kumwingiza samaki sangara kwenye Ziwa Victoria ambaye licha ya kuchochea viwanda kwenye eneo hilo bado dagaa wana nafasi kubwa zaidi kwa kiwango na uhakika wa chakula.

Hata hivyo FAO inasema ili kuhakikisha kuwa dagaa na samaki wengine wa maji baridi wanapatikana kwa kila mtu ni lazima kufanya mabadiliko ya kimsingi kiuchumi, kijamii na kisiasa kwenye maeneo kuanzia masoko, “kwa sababu mara nyingi huonekana kama ni taka na kuwavua, sheria zinasema ni kinyume cha sheria kwa kuwa wanaonekana ni uwepo wao ni muhimu ili kulinda samaki wakubwa.”

Mwandishi kiongozi wa nyaraka hiyo, Profesa Jeppe Kolding wa Chuo Kikuu cha Bergen, Norway amesema, "hali ya uvuvi kuelekea kwenye samaki wadogo kunaashiria kuweka mizani ya uvuvi na si ishara ya uvuvi wa kupindukia. Inadokeza kwamba uvuvi wa samaki wadogo kwenye maziwa na mito barani Afrika unaweza kuongezeka kwa uendelevu na hivyo ni fursa ya kipekee ya kukabili tatizo la njaa na lishe barani humo.”

FAO inapendekeza juhudi zaidi za kuwa na takwimu sahihi za uvuvi wa samaki hao wadogo, kutambua hasara za kupuuza thamani yao kiuchumi, kijamii na kwenye lishe na kuhamasisha mamlaka kuweka kanuni na mifumo ya kusongesha mifumo yenye uwiano ya uvuvi.