Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani mauaji katika jaribio la mapinduzi Ethiopia

Mwanamke kutoka Ethiopia akisali, dakika chache baada ya kuokolewa baharini akitoroka hali mbaya nchini mwake.
UNHCR/Hereward Holland
Mwanamke kutoka Ethiopia akisali, dakika chache baada ya kuokolewa baharini akitoroka hali mbaya nchini mwake.

UN yalaani mauaji katika jaribio la mapinduzi Ethiopia

Amani na Usalama

Mauaji ya kamanda mkuu wa jeshi na gavana nchini Ethiopia katika kile serikali inachosema kuwa ni jaribio la kikanda la mapinduzi yamelaaniwa vikali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo Jumapili Antonio Guterres amesema “ninatiwa hofu kubwa na mauaji  haya ya mwishoni mwa wiki”.

Gavana wa jimbo la kitaifa la Ambara aliuawa pamoja na mshauri wake akiwa mjini Addis ababa na mshirika mwingine mkubwa wa waziri mkuu wa Ethiopia ambaye ni mkuu wa majeshi ya nchi hiyo Jenerali Seare Mekonnen alipigwa risasi pamoja na afisa mwingine wa ngazi ya juu.

Guterres ametoa wito kwa wadau wote nchini Ethiopia kujizuia , kuzuia machafuko na kuepuka hatua zozote ambazo zitaathiti amani na utulivu nchini Ethiopia.

Kwa mujibu wa duru za habari, serikali imesema hivi sasa hali imedhibitiwa ambapo waziri mkuu amezungumza na taifa  kwa njia ya televisheni akiwataka Waethiopia wote kuungana dhidi ya uovu wa jaribio la mapinduzi la Amhara.

Jimbo la Amhara limekuwa na changamoto kubwa ya machafuko ya kikabila na serikali inaamini kwamba mauaji hayo yote mawili yanahusiana. Wengi wa wanaodaiwa kuhusika na jaribio hilo la mapinduzi wamekamatwa kwa mujibu wa ofisi ya waziri mkuu.

Waziri Mkuu wa Ethiopia amefanya mabadiliko mengi katika taifa hilo linalokuwa kwa kasi barani Afrika tangu alipochukua hatamu mwezi Aprili mwaka jana , akibadili uhusianao mbaya uliokuwepo na jirani zao Eritrea na kufanya mabadiliko makubwa ya serikali ya ndani.

Katibu Mkuu amesema katika taarifa yake kwamba “nakaribisha nia ya waziri mkuu na serikali ya Ethiopia ya kuhakikisha kwamba wahusika wa vitendo hivyo wanafikishwa mbele ya sheria.

Umoja wa Mataifa unaendelea kuwa tayari kuisaidia serikali  na juhudi zake za kushughulikia changamoto zinazoendelea.”

Takriban watu milioni 3 wametawanywa ndani ya ethiopia kutokana na migogoro ya muda mrefu ya kikabila ambayo mara nyingi huusisha umiliki wa ardhi na haki.