Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwasaidia wakimbizi na wenyeji wao, ni njia nzuri ya kuwahudumia watu waliotawanywa-Uganda

Wakimbizi wakiwa katika kituo cha afya kilichoko katika kambi yao ya Nakivale nchini Uganda
IRIN/Samuel Okiror
Wakimbizi wakiwa katika kituo cha afya kilichoko katika kambi yao ya Nakivale nchini Uganda

Kuwasaidia wakimbizi na wenyeji wao, ni njia nzuri ya kuwahudumia watu waliotawanywa-Uganda

Wahamiaji na Wakimbizi

Idadi ya wakimbizi wanaomiminika Uganda ikiripotiwa kila uchao, serikali ya Uganda imesema mkakati wa manufaa zaidi wa kuweza kusaidia kundi hilo ni lazima uweze kuwa na manufaa pia kwa wenyeji ambao kwa mujibu wa mfumo wa taifa hilo wanatangamana na wakimizi. 

Video iliyoandaliwa na Benki ya Dunia, kutoka angani inaonesha nyumba nyingi zilizosongamana katika eneo moja pana. Ni kambi ya wakimbizi Nakivale, iliyoko wilaya ya Isingiro kaskazini Magharibi mwa Uganda.

Wakimbizi na waliotawanywa nchini Uganda wamekuwa wakiongezeka, mathalani ndani ya mwaka mmoja wa 2017 waliongezeka kwa takribani mara tatu, kiasi cha kufikia takribani watu milioni moja nukta tano.

Wenyeji wanahangaika kuendana na hali hiyo na kwa upande wa serikali changamoto ni jinsi ya kuendeleza sera zake za kuwapatia wakimbizi fursa na wakati huo huo ikikabiliana na janga hili.

Maria Rosa Niwababega, mkimbizi kutoka Rwanda anasema, 

(Sauti ya Maria Rosa Niwabagega) 

“Nilipofika hapa nilikuwa nataka amani, nikae bila kusikia silaha au mtu wa kunikimbiza. Sasa ninatafuta labda wanipe usaidizi mwingine pengine wa kwenda nje sababu nilikimbia huko lakini maadui wanaweza kunikuta hapa. Au usaidizi wa pesa nifanye biashara ili watoto wangu wasome vizuri.”

Wakimbizi wanahitaji msaada kama ilivyo kwa jamii wenyeji ambao wanaishi katika hali duni. Dahir Nabbanja ni mwenyeji anayeishi karibu na kambi ya wakimbizi ya Nakivale, anasema,

(Sauti ya Dahir Nabbanja) 

“Sisi pia tunatakiwa kufikiriwa kwa kuwa hatujiwezi. Isingelikuwa chakula kiasi kinachosambazwa kwa wakimbizi ambacho pia ninapata kula, au mafuta ya kupikia ninayotumia, na vitu kama hivyo, ningelikuwa katika hali mbaya.”

Charles Bafaki ni Afisa katika kambi hiyo anayesimamia kitengo cha wakimbizi nchini Uganda anasema,

(Sauti ya Charles Bafaki) 

“Ili kuweza kutunza hali nzuri ya kimbilio katika hii nchi kuna haja ya kuishughulikia katika namna ambayo inasaidia jamii zote mbili, wakimbizi na wenyeji wao.”