Mfuko wa UN waleta nuru kwa maelfu ya manusura wa ukatili wa kingono

21 Juni 2019

Takriban watu 3,340 wakiwemo wanawake, watoto na wanaume wamenufaika na mfuko wa Umoja wa Mataifa wa kusaidia manusura wa vitendo vya ukatili wa kingono vilivyofanywa na wafanyakazi wa umoja huo.

Mfuko huo ulianzishwa mwaka 2016 ambapo hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New  York, Marekani mkuu wa Idara ya usimamizi wa mikakati na sera wa chombo hicho Jan Beagle ametoa taarifa kuhusu manufaa ya mfuko huo kwa kipindi cha miaka miwili sambamba na kupokea ahadi mpya kutoka kwa nchi wanachama.

“Katika kipindi hicho, wakati wa safari zangu, nimekuwa nikisumbuliwa na simulizi za kutisha za ukatili kutoka kwa wanawake, wasichana, wanaume na wavulana ambao wamekumbwa na ukatili wa kingono na zaidi ya yote kunyanyapaliwa wakati mwingine na jamii zao,” amesema Bi. Beagle wakati akifungua mkutano huo.

Hata hivyo amesema, “nimekuwa nikitiwa moyo na ujasiri na mnepo wao ambao  manusura hao wametumia kujenga upya maisha yao.”

Katika robo ya kwanza yam waka huu wa 2019 pekee, takwimu mpya zilizotolewa zinaonesha kuwa Umoja wa Mataifa umenukuu matukio 37 ya tuhuma za ukatili wa kingono na unyanyasaji, SEA uliofanywa na wafanyakazi wake, wakiwemo raia, wanajeshi na askari walio katika huduma ya ulinzi wa amani, mashirika ya Umoja wa Mataifa na miradi ya chombo hicho na kwamba hadi sasa tuhuma hizo zinachunguzwa.

Ni kwa mantiki hiyo Bi. Beagle amesema, “Umoja wa  Mataifa una wajibu wa kipekee wa kuweka viwango vya kimataifa vya kuzuia, kuchukua hatua na kutokomeza ukatili wa aina hii na kushughulikia madhara yake.

Kwa ainisho la Umoja wa Mataifa, “ukatili wa kingono ni kutekeleza au kutishia kumwingilia mtu kingono iwe kwa nguvu au kwa mazingira ya shinikizo.

Unyanyasaji wa kingono kwa upande wake ni “tukio lolote au jaribio lolote la matumizi mabaya ya mazingira hatarishi ya mtu, au mamlaka au imani yake kwako kwa manufaa ya kingono, ikiwemo kujinufaisha kifedha, kijamii au kisiasa kwa kumnyanyasa mtu kingono.”

United Nations
Kipeperushi kikionesha nchi wachangiaji wa mfuko huo wa usaidizi wa manusura wa ukatili na unyanyasaji wa kingono pamoja na maeneo ya miradi.

Mfuko wa kurejesha utu

Mfuko wa kusaidia manusura wa ukatili na unyanyasaji wa kingono ni moja ya mikakati iliyoanzishwa na Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka iliyopita ili kushughulikia makovu ya ukatili huo ndani ya mfumo wa Umoja wa Mataifa.

Lengo la mfuko ni kusaidia kifedha manusura na watoto wanaozaliwa kutokana na ukatili wa kingono unaofanywa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

Tangu mwaka 2016, jumla ya dola milioni 2 zimepatiwa mfuko huo na kuwezesha kutekeleza miradi kadhaa ya uwezeshaji manusura.

Hadi sasa, kiasi kikubwa cha fedha kimekusanywa kutokana na michango ya wanachama 19 wa Umoja wa Mataifa. Takribani dola 400,000 ni malipo ya wafanyakazi wa  Umoja wa Mataifa ambao madai yao ya kutekeleza ukatili wa kingono yamethibitishwa.

Miradi inayotekelezwa na mfuko huo

Miwili, ni katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, miradi ambayo inasaidia jamii kujipatia kipato sambamba na mfumo wa kuweza kuwasilisha malalamiko ya ukatili wa kingono.

 

Halikadhilika miwili nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ambapo miradi itawapatia manusura msaada wa kisheria kwa miaka miwili ijayo.

Na nchini Liberia kuna mradi mmoja.

Kwa mujibu wa Bi. Beagle “mapendekezo ya nyongeza kwa miradi yamewasilishwa na sasa yanafanyiwa mapitio au yameshapitishwa na ni kwa ajili ya DRC, Haiti, Sudan Kusini na CAR.”

Akiangazia kile walichojifunza kutokana na utendaji wa mfuko huo kwa kipindi cha miaka miwili sasa, Bi. Beagle ametaja mambo makuu matatu ambayo ni mosi, umuhimu wa mfuko kupatia kipaumbele manusura, pili, umuhimu wa mfuko kuendana na mazingira na utoaji fedha usiokuwana ukomo kutoka kwa nchi wachangiaji na tatu ni umuhimu wa kujumuisha miradi mipya kwenye miradi ya zamani badala ya kuanzisha mipya kabisa.

Je pengo litashughulikiwa vipi?

Mchechemuzi wa haki za manusura wa ukatili na  unyanyasaji wa kingono, Jane Connors naye akapaza sauti akisema kuwa ukatili na unyanyasaji wa kingono kutoka kwa watendaji wa Umoja wa Mataifa ni udhaifu wa chombo hicho. “Hii leo miradi imelenga kwenye maeneo ya ulinzi wa amani na kwenye jumbe za Umoja wa Mataifa, lakini kwa kusonga mbele lazima wigo uwe mpana zaidi hata kwa manusura walio kwenye maeneo mgngine.”

Hivi sasa, ofisi ya mchechemuzi huyo inaandaa wigo wa usaidizi kwa manusura ikiwemo wa kisheria, tiba, usalama, makazi na jinsi ya kuinua vipato vyao katika mataifa manane, na huduma hiyo itaenezwa kwenye nchi zingine.

Sasa SEA ishambuliwe kutoka kona zote- Guterres

Mwaka 2017, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alizindua mkakati wake, unaojikita katika kushughulikia ukatili na unyanyasaji wa kingono kwenye mfumo wa Umoja wa Mataifa, ikihusisha walinda amani pamoja an wale wote waliopewa mamlaka ya kutekeleza miradi ya  Umoja wa Mataifa kama ile ya Baraza la Usalama lakini wasio wanajeshi.

Hii ni jumla ya watendaji 90,000 walioko kwenye vyombo zaidi ya 30 pamoja na wanajeshi 100,000.

Akihutubia kwenye mkutano wa leo, Naibu Mkuu wa masuala ya siasa kwenye Umoja wa Mataifa Miroslav Jenča, ameeleza kuwa Umoja wa Mataifa unakabiliana na SEA kupitia pembe tatu.

Mosi ni kuzuia, ambapo kabla ya kwenda kwenye operesheni kuna mafunzo ya lazima kwa wanajeshi wote.

Pili ni kusimamia sheria kupitia kuwepo kwa mifumo ya kupokea malalamiko na mchakato wa nidhamu ili kuwajibisha wahusika,

Tatu ni kutoa msaada ikiwemo kwa manusura.

Katika kushughulikia pembe ya tatu, Bwana Jenča amesema kuwa, “mbinu ya msingi kusongesha suala hilo ni kupitia mfuko wa usaidizi kwa manusura na watoto waliozaliwa.”

Bwana Jenča ameshukuru nchi wanachama zinazosaidia mfuko huo akisema zinawapatia sauti wasio na sauti.

 

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud