Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio la karne la ILO lisiwe tu ahadi bali litekelezwe kwa kuzingatia utu wa binadamu- Guterres

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia mkutano wa 108 wa Baraza la shirika la kazi duniani, ILO mjini Geneva, Uswisi hii leo 21 Juni 2019
UN /Jean-Marc Ferré
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia mkutano wa 108 wa Baraza la shirika la kazi duniani, ILO mjini Geneva, Uswisi hii leo 21 Juni 2019

Azimio la karne la ILO lisiwe tu ahadi bali litekelezwe kwa kuzingatia utu wa binadamu- Guterres

Masuala ya UM

Mkutano wa 108 wa Baraza la shirika la kazi duniani, ILO ukikunja jamvi kwa kupitisha azimio la karne kufuatia shirika hilo kutimiza miaka 100, Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema nyaraka hiyo ni fursa mpya ya kufungua mustakabali bora zaidi kwa wakazi wa dunia.

Akihutubia hii leo wajumbe kwenye mkutano huo ulioanza mjini Geneva, Uswisi tarehe 10 mwezi huu wa Juni,  Katibu Mkuu amesema, “azimio hilo lina matarajio makubwa, likiweka msingi wa jinsi ya ILO itatekeleza majukumu yake katika karne yake ya pili.”

Hata hivyo amesema, “nyaraka hii ya karne ni zaidi ya maelezo ya matamanio au nia. Inapendekeza kubadili mtazamo wetu kuhusu maendeleo. Ustawi wa watu ni lazima uwe kitovu cha sera za kiuchumi na kijamii na lazima tuangazie zaidi wale ambao wameacha nyuma zaidi, wakiwemo watu wenye ulemavu, watu wa jamii ya asili, wazee, wanawake na vijana walio hatarini.”

Mkataba wa kupiga marufuku ghasia makazini

Katibu Mkuu ametumia hotuba yake kupongeza kupitishwa kwa mkataba aliosema wa aina yake wa kupiga marufuku ukatili na manyanyaso sehemu ya kazi.

Mkataba huo uliopitishwa kwa kura 439, huku nchi 7 zikipinga na 30 hazikupiga kura yoyote, unatambua kuwa ghasia na manyanyaso kazini ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Akigusia kuwa zama za sasa zina changamoto nyingi pamoja na hata walio kwenye ajira wanakumbwa na changamoto hizo, Katibu Mkuu amesema, “msingi ongozi kwenye kazi yetu lazima iwe kusongesha  utu wa kibinadamu.”

Watoto na watu wazima kutoka Romania wakifanyakazi katika eneo la kutupa taka jirani na makazi ya Nadezhda nchini Bulgaria. Familia hizi zinakosa fursa za ajira, ambayo ndio kauli mbiu ya ripoti ya mwaka huu ya ILO kuhusu mtazamo wa ajira na mwenendo Duni
UNICEF
Watoto na watu wazima kutoka Romania wakifanyakazi katika eneo la kutupa taka jirani na makazi ya Nadezhda nchini Bulgaria. Familia hizi zinakosa fursa za ajira, ambayo ndio kauli mbiu ya ripoti ya mwaka huu ya ILO kuhusu mtazamo wa ajira na mwenendo Duni

Ushirikiano wa kimataifa

“Zaidi ya zaidi, tunahitaji majibu ya pamoja kushughulikia changamoto za dunia. Lakini zaidi na zaidi ushirikiano wa kimataifa  unashambuliwa kuliko,” amesema Guterres akiongeza kuwa matatizo yanayokumba dunia hivi sasa ni magumu kuliko huku suluhu zikiwa ni za vipande vipande.

Kama hiyo haitoshi, amesema kila pahali, imani inazidi kutoweka na hofu inajengeka zaidi na zaidi, “unaweza kuita ni zama za kukata tamaa.”

Kwa mantiki hiyo amesema njia bora zaidi ni kujenga imani kwa kusikiliza watu na kujibu shida zao.

“Shirika la kazi duniani, lina dhima kuu kwa sababu kuu, ajenda yenu inagusa watu. Utu kwenye ajira. Utandawazi ulio na usawa, haki ya kijamii kwa kila mtu kila pahali,” amesema Guterres.

Amekumbusha ILO kuwa kuleta mabadiliko na kuzingatia masuala hayo ni jambo la kawaida kwa ILO.

Mtoto wa Kiindonesia katika ajira ya watoto kwenye uvuvi na utengenezaji viatu
ILO/Asrian Mirza
Mtoto wa Kiindonesia katika ajira ya watoto kwenye uvuvi na utengenezaji viatu

Kazi na Mazingira

Kuhusu mustakabali wa utendaji kazi duniani Katibu Mkuu amegusia azimio hilo ambalo linaangazia uhusiano wa changamoto zilizopo akisema kuwa, “hatuwezi kuwa na mustakabali bora wa kazi bila kuwa na uendelevu wake. Na hatuwezi kuwa na mustakabali bora bila kushughulikia changamoto ya tabianchi.”

Hivyo amekumbusha suala la kazi au ajira ambazo haziharibu mazingira, akisema ni lazima zipatiwe kipaumbele katika harakati zozote zile za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi akitanabaisha kuwa, “tunahatarisha mustakabali wetu kwa kuongeza ukosefu wa utulivu, ukosefu wa usawa na umaskini.”

Guterres akakumbusha wajumbe mkutano kuhusu tabianchi alioitisha mwezi Septemba mjini New York, Marekani akitaka wajumbe waje na maamuzi ya kina na yenye kuleta mabadiliko chanya dhidi ya mwenendo wa sasa wa tabianchi.