Machafuko yalazimisha watoto 600,000 kukosa elimu Cameroon:UNICEF

21 Juni 2019

Zaidi ya asilimia 80 ya shule zimefungwa katika majimbo ya Kaskazini Magharibi na Kusini magharibi mwa Cameroon kufuatia machafuko yanayoendelea na kuwalazimisha watoto zaidi ya 600,000 kukosa fursa ya elimu  limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo imeainisha kuwa watu wengine milioni 1.3 wakiwemo watoto 650,000 hivi sasa wanahitaji msaada wa kibinadamu kwenye majimbo hayo ambapo hali ya usalama na maisha vinaendelea kudorora.Watu 450,kati ya hao ni wakimbizi wa ndani na nusu yao ni wanawake na watoto.

Kwa mujibu wa UNICEF “watoto na familia zao wanateseka na kulazimika kukimbia vita, mashambulizi katika nyumba zao na shuleni, kutekwa , ukatili wa kingono na kushinikizwa na makundi yenye silaha kuingia jeshini kushiriki vita.”

Pia shirika hilo limeongeza kuwa hali ya watu kutoruhusiwa kutembea au kutoka nnje kwa siku kadhaa kutokana na amri iliyowekwa na makundi yenye silaha inaathiri uhuru wa watu wa kutembea na wahudumu kufikisha misaada ya kibinadamu inayohitajika.

UNICEF imesema maelfu ya watu hatika majimbo ya Kaskazini Magharibi na Kusini Magharibi mwa Cameroon hawana au wanapata huduma kidogo sana ya masuala ya msingi kama huduma za afya, maji salama ya kunywa na maisha yao yamesambaratishwa. Tangu Disemba mwaka 2018 inakadiriwa kwamba asilimia 40 ya vituo vya afya vya jimbo la Kusini Magharibi havifanyi kazi.

Mgogoro ulianza kutokana na maandamano ya watu kutoka sehemu wanayozungumza Kiingereza nchini humo wakihitaji mamlaka zaidi yapata miaka mitatu iliyopita na mgogoro huo umekuwa na athari kubwa kwa watoto hasa haki yao ya kupata elimu. Kwa mujibu wa UNICEF”Kwa watoto wengi imekuwa ni miaka mitatu tangu walipotia mguu darasani. Kutokana na marufuku ya elimu iliyowekwa na makundi yenye silaha na mashambulizi , ambapo zaidi ya asilimia 80 ya shule zimefungwa na kuathiri watoto zaidi ya laki sita. Shule 74 zimesambaratishwa kabisa na mashambulizi, huku wanafunzi, waalimu na wahudumu wengine wa shule wakikabiliwa na ghasia, kutekwa na vitisho.Tangu mwaka 2018 wanafunzi na waalimu Zaidi ya 300 walitekwa na baada ya kupitia madhila makubwa wakaachiliwa.”

UNICEF inasema kulenga elimu ni kuweka njia panda mustakbali wa kizazi chote cha watoto wa maeneo hayo ambao kwa kupatiwa msaada sahihi na fursa wanaweza kujenga mustakabali imara na bora wenye matumaini.

Wakati fursa za wahudumu wa misaada kuwafikia waathirika zikiendelea kuwa changamoto , UNICEF na wadau wake wanafanya kila wawezalo kuwafikia na kuimarisha maisha ya watoto na watu wenye mahitaji.

Takribani watoto 15, 000 waliotawanywa na machafuko , UNICEF inasema hivi sasa wanahudhuria shule katika jamii zinazowahifadhi nje ya majimbo hayo na waalimu wamepatiwa mafunzo ili kuwapatia watoto hao msaada wa kisaikolojia kutokana na madhila waliyopitia.

Kwa sasa UNICEF inahitaji dola milioni 20 kuweza kukabiliana na dharura iliyoko katika majimbo hayo kwa mwaka huu.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud