Sheria mpya Ethiopia kuwanufaisha wakimbizi

21 Juni 2019

Ethiopia ni mwenyeji wa wakimbizi takribani laki tisa ambao wengi wao wanaishi katika kambi, na mara nyingi hawana haki ya kufanya kazi au kutembea kwa uhuru, lakini sasa mambo yanabadilika. Sheria mpya ya wakimbizi itawafanya wakimbizi wawe na fursa nyingi zaidi. 

Ethiopia imekuwa ikipokea wakimbizi wengi hususani kutoka Eritrea. Wengi wa wakimbizi hao wako kambini lakini wachache kati yao tayari wameruhusiwa kuishi mjini na kuanzisha biashara.

Ahmedin Ibrahim ni mkimbizi  kutoka Eritrea. Amehama hivi karibuni kutoka katika kambi ya wakimbizi akiwa na watoto wake sita na sasa anaendesha karakana yake ya kutengeneza samani katika eneo la Shire, Ethiopia, anasema

“Ni vizuri kujipatia kipato mwenyewe kuliko kutegemea misaada kutoka kwa wengine.”

Ahmed ameongeza kuwa Watoto wake, wakiwemo mabinti zake, wanafanya kazi kwa pamoja, 

“Inawasaidia kusimama kwa miguu yao miwili na kujihudumia wenyewe badala ya kutegemea kutoka kwangu.”

Eyob Awoke ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa masuala ya wakimbizi na wanaorejea nyumbani kutoka ukimbizini ARRA anasema,

“Maono yetu ni kuwa katika kipindi cha miaka kumi tuwe tumeondokana na kambi za wakimbizi. Wakimbizi ni raslimali hususani wanapokuwa katika idadi kubwa kama hawa waliopo Ethiopia. Wakijihusisha katika masuala kadhaa ya kijamii itakuwa faida kwa pato la taifa.”

Umoja wa Mataifa unaendelea kuzisihi nchi kote duniani, pamoja na kuzuia vita, pia zifungue mipaka yake ili kuwapokea wakimbizi na pia kuwapa fursa kushiriki katika shughuli za kijamii.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter