Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano yakiendelea Tripoli, wakimbizi 131 wasafirishwa kwenda Niger

Watu walioshikiliwa kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli, wakisubiri kuhamishiwa eneo salama. Pichani Msichana kutoka Eritrea mwenye umri wa miaka 19 akizungumza na mfanyakazi wa UNOCHA akisubiri kupanda basi kuelekea kituo cha mpito kabla ya kwenda Niger.
UN OCHA/GILES CLARKE
Watu walioshikiliwa kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli, wakisubiri kuhamishiwa eneo salama. Pichani Msichana kutoka Eritrea mwenye umri wa miaka 19 akizungumza na mfanyakazi wa UNOCHA akisubiri kupanda basi kuelekea kituo cha mpito kabla ya kwenda Niger.

Mapigano yakiendelea Tripoli, wakimbizi 131 wasafirishwa kwenda Niger

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati mapigano yakiendelea kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli, wakimbizi 131 jana usiku wamesafirishwa kutoka mjini humo kwenda kituo cha dharura cha hifadhi, ETM kilichopo nchini Niger.

 

Miongoni mwao ni kutoka Eritrea, Somalia na Sudan, wakiwemo watoto 65 wenye umri wa chini ya miaka 18.
Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR imesema baadhi yao wamekuwa wakishikiliwa korokoroni mjini Tripoli kwa zaidi yam waka mmoja.

“Hatuwezi kuchukulia kimzaha umuhimu wa misafara hii ya kwenda Niger,” amesema Jean-Paul Cavalieri, mkuu wa ofisi ya UNHCR nchini Libya akisema kuwa, “katika siku ya wakimbizi duniani hii leo, wakimbizi hawa wataweza kulala wakitambua kuwa wao na familia zao hawapo tena hatarini.”

Hata hivyo amesema hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa akisema, “serikali lazima ziongeze usaidizi wao katika kusaidia kuhamisha wakimbizi walio hatarini nchini Libya.”

Kabla ya kusafirishwa, wakimbizi hao walikuwa wamehifadhiwa kwenye kituo cha UNHCR cha kusubiria safari, GDF, kilichopo mjini Tripoli.

UNHCR imetoa shukrani zake kwa Wizara  ya mambo ya ndani ya Libya pamoja na shirika la LibAid ambao kwa pamoja walisaidia kufanikisha kuachiliwa kwa watu hao na kusafirishwa hati vituo vya safari.

Katika kituo hicho cha GDF, wakimbizi hupatiwa chakula, malazi, matibabu ikiwemo ya kisaikolojia pamoja na nguo na vifaa vya kujisafi.

Wakiwa Niger, wakimbizi hao wakati wanasubiri mpango wa kuhamishiwa nchi ya tatu, watapatiwa misaada ya kibinadamu.

Safari ya jana usiku imefanya idadi ya watu waliohatarini nchini Libya waliohamishwa na UNHCR mwaka huu pekee kufikia 1,297 ambapo kati yao 711 wameenda Niger, 295 wameenda Italia na 291 wamepata makazi ya tatu Ulaya na Canada.