Matibabu ya kifafa bado ni shida kubwa kwa nchi za kipato cha chini- WHO

20 Juni 2019

Robo tatu ya watu walio na ugonjwa waa kifafa katika nchi zenye kipato cha chini hawapati matibabu wanayoyahitaji na hivyo kuongeza hatari ya kufa kabla ya wakati wao, imesema ripoti mpya ya shirika la afya duniani WHO.

Utafiti huo umezinduliwa leo na WHO kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali katika masuala ya ugonjwa wa kifafa.

Dkt Tarun Dua wa kitengo cha afya ya akili na matumizi mabaya ya dawa cha WHO amesema, “pengo la matibabu ya kifafa ni kubwa mno, wakati tunafahamu kuwa asilimia 70 ya watu wenye kifafa wanaweza kukumbwa na kuanguka kwa kifafa wanapokuwa kwenye nafasi ya kupata dawa ambayo inagharimu kiasi kidogo cha fedha kama dola 5 tu za kimarekani kwa mwaka mzima na zinaweza kufikishwa kupitia mifumo ya msingi ya afya.”

Kifafa husababisha vifo vya mapema

Ripoti hiyo ya WHO inaendelea kueleza kuwa uwezekanao au hatari ya kifo cha mapema kwa watu wenye kifafa ni mara tatu zaidi kuliko kwa watu wasio na tatizo hilo ambapo katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, vifo vya mapema miongoni mwa watu wenye kifafa ni vingi zaidi kuliko katika nchi zenye kipato kikubwa. 

Sababu za vifo hivyo zinahusishwa na uhaba wa huduma za kiafya wakati mgonjwa anapoanguka au matukio ya kuanguka yanapofuatana na pia sababu nyingine zinazozuilika kama vile kuzama majini, kujeruhi kichwa na kuungua.

Aidha ripoti imefafanua kuwa kwa kakribani nusu ya watu wazima wenye tatizo la kifafa wana angalau shida nyingine moja ya kiafya. Kwa watoto wenye kifafa takribani asilimia 30 hadi 40, wanakumbana na ugumu katika kukua kiakili na uwezo wa kujifunza.

Unyanyapa ni kikwazo

Unyanyapaa dhidi ya watu wenye kifafa umetajwa kuwa ni mkubwa ambapo Dkt Martin Brodie rais wa shirika la International Bureau for Epilepsy, IBE anasema, “unyanyapaa unaohusishwa na kifafa ni moja ya sababu kubwa zinazowazuia watu katika kutafuta matibabu. Watoto wengi wenye kifafa hawaendi shuleni na watu wazima wananyimwa kazi, haki ya kuendesha vyombo vya usafiri na hata kuoa na kuolewa. Uminyaji huu wa haki hizi za binadamu wanaokumbana nao watu wenye kifafa vinapaswa kukoma.”

Wataalamu hao wa afya wameeleza kuwa asilimia 25 ya visa vya kifafa vinaweza kuzuilika na pia wakazitaja sababu za kifafa kuwa ni pamoja na mtoto kupata msukosuko kwenye ubongo wakati anazaliwa,  maambukizi ya ubongo na kupooza. Inaelezwa kuwa takribani watu milioni 50 wenye umri tofauti tofauti kote duniani wameathirika na kifafa.

 

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter