Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres hatazingatia pendekezo la kuunda chombo kuchunguza mauaji ya Khashoggi-UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa António Guterres
UNFCCC Secretariat/James Dowson
Katibu Mkuu wa Umoja wa Matafa António Guterres

Guterres hatazingatia pendekezo la kuunda chombo kuchunguza mauaji ya Khashoggi-UN

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema atazingatia pendekezo moja tu miongoni mwa mapendekezo yaliyoelelezwa kwake na ripoti iliyotolewa leo kuhusu mauaji ya mwanahabari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, amesema hayo hii leo jijini New York, Marekani wakati alipoulizwa swali na waandishi wa habari iwapo Katibu Mkuu atazingatia mapendekezo hayo ikiwemo ya kuanzisha uchunguzi wa kimataifa wa mauaji ya mwanahabari hayo.

“Ripoti hiyo ya mtaalamu huru ina mapendekezo mengi kwa vyombo kadhaa na yakitaka hatua tofauti. Kwa upande wake, Katibu Mkuu atazingatia kikamilifu pendekezo kuhusu ulinzi wa wanahabari, suala ambalo amekuwa akilipigia chepuo kila wakati,” amesema Bwana Dujarric.

Msemaji huyo ameongeza kuwa, “kuhusu mauaji ya Khashoggi, Katibu Mkuu anaamini kuwa ulikuwa ni  uhalifu wa kikatili ambao ulishtua watu wengi duniani,” na kwamba tangu ripoti za awali kuhusu mauaji hayo zilipotangazwa, “Katibu Mkuu amelaani kwa uwazi kabisa na kutoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa wazi, haraka na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.”

Bwana Dujarric amesema kuwa huo ndio umesalia msimamo wa Katibu Mkuu akiongeza kuwa, “Katibu Mkuu hana mamlaka ya kuanzisha uchunguzi wa kihalifu bila mamlaka kutoka chombo cha kiserikali chenye ueledi. Mamlaka hayo yako chini ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.”

Msemaji huyo ameongeza kuwa iwapo uchunguzi kamili na wa dhati hautaitishwa na nchi wanachama, nji peke ya kufanya  uchunguzi huo, ikihitaji ushirikiano kutoka kwa nchi husika wanachama, itakuwa kupitia, “azimio la Baraza la Usalama kwa mujibu wa vipengele sahihi vya Katiba ya Umoja wa Mataifa.”

Amesisitiza kuwa ni lazima nchi zote wanachama zishirikine kwenye juhudi hizo.