Saudi Arabia inahusika na mauaji ya Khashoggi-Mtaalamu wa UN

19 Juni 2019

Mwandishi wa habari wa Saudia Jamal Khashoggi alikuwa mwathirika wa mauaji ya kupangwa ambayo Saudia Arabia inahusika nayo, imesema ripoti iliyotolewa hii leo mjini Geneva na mtaalamu wa haki za binadamu  wa Umoja wa Mataifa anayefuatilia hukumu zisizofuata sheria na pia mauaji ya kiholela, Agnes Callamard.

Kufuatia uchunguzi uliodumu kwa miezi sita, Bi. Callamard ametoa matokeo kuhusu kuuawa kwa Khashoggi katika ubalozi wa Saudia mjini Istanbul Uturuki akionesha ushahidi kwa mujibu wa vigezo vya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu pia hatua ambazo zingezuia mauaji hayo.

Sehemu ya ripoti hiyo inasema, “mazingira ya kifo cha Khashoggi yamesababisha nadharia nyingi na madai lakini hakuna hata moja inaondoa kuhusika kwa Saudi Arabia. Mawakala wa Saudia, kumi na tano kati yao walifanya njama za siri na wakatumia mazingira ya serikali kumuua Bwana Kashoggi.Kuuawa kwake kulikuwa matokeo ya mipango Madhubuti ya kibinadamu na kifedha. Ilipangwa vizuri na iliidhinishwa na viongozi wa juu.”

Aidha ripoti hiyo imeonesha maeneo sita ya ukikukwaji wa sheria za kimataifa ikiwemo sheria inayozuia mauaji ya kiholela, matumizi makubwa ya nguvu, na sheria dhidi ya mateso.

Mtaalamu huyo wa haki za binadamu anasema pia kuwa kuna ushahidi wa kuaminika, uchunguzi zaidi wa kuhusika kwa viongozi wa Saudia akiwemo mwana mfalme wa nchi hiyo.

Callamard ametoa wito kwa Baraza la haki za binadamu, Baraza la Usalama au Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kufanya uchunguzi wa kimataifa kwa minajili ya kubaini kuhusika kwa kila mtu na pia njia za kufuata kuelekea kuwajibika kisheria.

Vilevile ripoti hiyo imeitaka Saudi Arabia iwaachie huru watu wote waliofungwa kutokana na kutoa maoni yao au wanachokiamini na pia kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya wahusika, taasisi na mazingira yote yaliyosababisha kuuawa kwa Khashoggi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud

Fuatilia Habari: Habari zilizopita za Mada Hii

Taarifa za kifo cha Khashoggi zimenisikitisha:Guterres 

Baada ya sintofahamu ya muda leo serikali ya Saudia Arabia imethibitisha kuwa mwanahabari JamalKhashoggi aliyetoweka tangu tarehe pili Oktoba , amefariki dunia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema amesikitishwa na taarifa hizo na anataka uchunguzi wa kina ufanyike.

Chunguzeni kupotea kwa Khashoggi huko Uturuki- Wataalamu UN

Wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wameeleza wasiwasi wao mkubwa juu ya taarifa za kutoweka kwa mwandishi wa habari wa Saudi Arabia nchini Uturuki, ambaye hakusita kuikosoa serikali alipohisi inakwenda kombo.