Ukisikia hadithi za wakimbizi itakuwa vigumu kuwachukia:Mkimbizi Mustafa

19 Juni 2019

Kuwa mkimbizi ni hali ambayo mara nyingi sio chaguo bali ni lazima kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita, njaa na hata mateso. Katika kuelekea siku ya wakimbizi duniani itakayoadhimishwa hapo kesho Juni 20 sikiliza safari ya Mustafa mkimbizi kutoka Somalia aliyepoteza baba yake na sasa anaishi hapa Marekani 

Huyu ni Mustafa mkimbizi kutoka nchi Somali akisema ukihadithiwa madhila wanayopitia wakimbizi si rahisi kuwachukia. Yeye na familia yake wakimbia Somalia baada ya kupoteza baba yake sababu ya vita na kuishi kambini Kakuma Kenya kwa miaka 8. Mustafa anasema, “tulipokwenda katika safari hii nilikuwa na umri wa miaka 11 tu, na inabidi uache kuwa mtoto na ghafla unaanza kufikiria kama mtu mzima kwa sababu huna chaguo.”

Mwaka 2014 kupitia mpango wa shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi UNHCR wa kuwahamishia wakimbizi nchi ya tatu ukamleta yeyé na familia yake na kuwapa makazi Lancaster Pennsylvania hapa Marekani. Ndipo Mustafa akaja na wazo ambalo alikumfurahisha kila mtu, "nilipokuja Marekani nikabaini kwamba masuala ya wakimbizi yamefanywa kuwa ya kisiasa hivyo nikaanza kuchapisha kwenye Facebook, inamaanisha nini kuwa mkimbizi, na nikaanza kupokea ujumbe kutoka kwa mtu anayeitwa Mark akinijibu vibaya na kusema Marekani haitaki wakimbizi, nikamjibu na kuwambia hey tunaweza kukutana kunywa kahawa, tukakutana na kwa dakika 10 hivi tukazungumza masuala ya wakimbizi.”

Mkutano wao ulibadili kabisa mtazamo wa Mark na kufungua mlango mwingine kwa Mustafa  wa kuanzisha jukwaa la kukutanisha wakimbizi na wenyeji na kwamba “hapo ndipo nilipata wazo la kuanzisha bridge ambalo unaweza kukutanisha watu wa tamaduni mbalimbali na wakimbizi wa eneo hilo, kusikiliza hadithi zao na kufurahia chakula chao na kujenga jamii”

Bridge ni mpango wa chakula cha familia ambacho hukutanisha wenyeji na wakimbizi na kuzungumza na kusimulia inamaanisha nini kuwa mkimbizi. Hadi sasa watu 3000 wamefurahia chakula na kukutana katika mpango wa Bridge.

Na kwa Mustafa, "ninachotaka kila mtu ajue kuhusu kuwa mkimbizi ni kwamba sisi ni watu tunaopitia hali ambayo hatukuichagua lakini tunamatumini kuhusu Maisha , tuna mnepo, na wakimbizi ni watu kama watu wengine ambao ni jirani zako na utakapojua hadithi zao itakuwa vigumu kuwachukia.”

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter