Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili wa kingono katika mizozo ni msalaba wetu sote:UN

Wanafunzi nchini Sudan Kusini wakigiza suala la ukatili wa kingono katika maeneo yenye mizozo.
UNMISS/Isaac Billy
Wanafunzi nchini Sudan Kusini wakigiza suala la ukatili wa kingono katika maeneo yenye mizozo.

Ukatili wa kingono katika mizozo ni msalaba wetu sote:UN

Amani na Usalama

 Ukatili wa kingono katika mizozo ni tishio kwa usalama wetu sote na ni doa katika utu wetu amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres. 

Kupitia ujumbe wake maalumu wa siku ya kimataifa kwa ajili ya kutokomeza ukatili wa kingono katika mizozo Guterres amesema ukatili huo unatumika kama mbinu ya vita kutisha watu na kusambaratisha jamii na kwamba

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

Athari zake zinaweza kwenda vizazi na vizazi kupitia madhila, unyanyapaa, umasikini, athari za kiafya za muda mrefu na mimba zisizotakikana. Katika siku ya kimataifa kwa ajili ya kutokomeza ukatili wa kingono katika mizozo tunapaswa tuwasikilize waathirika na kutambua mahitaji na matakwa yao.”

Ameongeza kuwa wengi wa waathirika hao ni wanawake na wasichana lakini pia wanaume na wavulana, ambao wanahitaji msaada ili kupata huduma za afya za kuokoa maisha yao, kujikimu kimaisha, haki na fidia.

Na kwa mantiki hiyo Umoja wa Mataifa katika operesheni zake mbalimbali umeanzisha mafunzo maalum kwa ajili ya waathirika hao mathahalani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, kupitia mpango wake nchini MONUSCO. Mafunzo hayo ni ya ujasiriamali wa aina mbalimbali kuanzia ufugaji, upishi, kuoka mikate, na hata ushonaji. Miongoni mwa waliofaidika na miradi hiyo ni kina mama hawa muoka mikate na fundi cherahani

(SAUTI YA WAATHIRIKA.)

Umoja wa Mataifa unasema katika kuadhimisha siku hii pia tunawaenzi ambao wanafanyakazi mstari wa mbele, wakiwasaidia moja kwa moja waathiri ili kujenga upya maisha yao. 

Katibu Mkuu ametoa wito kwamba hatua za pamoja lazima zijumuishe maamuzi ya pamoja ili kuhakikisha uwajibikaji kwa waliotekeleza ukatili huo na kushughulikia kutokuwepo usawa wa kijinsia ambao unachochea maovu haya kwani kwa pamoja dunia inaweza na inapaswa kubadili ukwepaji sheria kwa kuweka haki, na kutofautiana kwa kuchua hatua.