Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Misri chunguzeni kwa kina na kwa huru  mazingira ya kifo cha Morsi

Mohamed Morsi, enzi za uhai wake na wakati akiwa Rais wa Misri alipokuwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
UN /Marco Castro
Mohamed Morsi, enzi za uhai wake na wakati akiwa Rais wa Misri alipokuwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa

Misri chunguzeni kwa kina na kwa huru  mazingira ya kifo cha Morsi

Haki za binadamu

Ofisi ya Kamishna mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa imesema ni matumaini  yake kuwa uchunguzi huru na wa kina utafanyika juu ya mazingira ya kifo cha Rais wa zamani wa Misri, Mohamed Morsi kilichotokea jana wakati akiwa mahakamani.

Msemaji wa ofisi hiyo, Rupert Colville amesema hayo kupitia taarifa iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi, baada ya ripoti ya kwamba hapo jana Morsi, rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri, kuzimia wakati kesi yake ikiendelea mahakamani na hatimaye kuelezwa kuwa amefariki dunia.

“Kwa kuwa rais huyo wa zamani alikuwa korokoroni chini ya mamlaka za Misri wakati wa kifo chake, serikali inawajibu wa kuhakikisha kuwa alitendewa kiutu na kwamba haki yake ya uhai na afya ziliheshimiwa,” amesema Bwana Colville.

Amesema kifo chochote cha ghafla wakati mtu yuko rumande kinapaswa kufuatiwa na uchunguzi wa haraka, wa kina na huru na ulio wazi ambao utafanywa na chombo kilicho huru ili kubainisha sababu za kifo.

“Hizi ni kanuni zilizoainishwa na vyombo vya haki za binadamu, ikiwemo Kamisheni ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa ambayo sote tunakubaliana nayo,” amesema msemaji huyo.

Ameongeza kuwa serikali, ikiwemo Misri ambazo zimeridhia agano la haki za kiraia na kisiasa zina wajibu wa kuchukua hatua muhimu kulinda maisha ya wale waliopokwa uhuru wao akisema kuwa, “kwa kukamata, kushikilia, kufunga au vinginevyo  kumnyima mtu uhuru wake, nchi wanachama wa agano hilo zinakuwa zimewajibika kulinda uhai wa mhusika.”

Ofisi hiyo imetoa taarifa hiyo kufuatia wasiwasi ulioibuka juu ya mazingira aliyokumbana nayo Morsi wakati akiwa anashikiliwa ikiwemo kukosa matibabu sahihi pamoja an kushindwa kukutana na mawakili na familia yake katika kipindi chote cha miaka 6 aliyokuwa korokoroni.

Kwa mantiki hiyo ofisi hiyo imesema uchunguzi huo ni lazima uangalie mazingira yote ya jinsi alivyotendewa na uangalie pia iwapo mazingira alimokuwa anashikiliwa yalikuwa chanzo cha kifo chake.