Timu ya Sampdoria yaleta matumaini kwa wakimbizi na wenyeji Uganda

18 Juni 2019

Nchini Uganda, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kwa kushirikiana wadau mbalimbali ikiwemo kamati ya kimataifa ya olimpiki, IOC na ubalozi wa Italia nchini humo wamewezesha klabu ya soka nchini Italia, Sampdoria kuleta nuru kwa wakimbizi kupitia mchezo wa soka.

UNHCR kupitia makala iliyochapishwa kwenye wavuti wake imesema makocha wawili wa klabu hiyo iliyodumu kwa miaka 73 sasa wameendesha kambi na wakimbizi na wenyeji ikijumuisha jumla ya watu 64.

Miongoni mwao ni Patrick Amba mkimbizi kutoka Sudan Kusini ambaye amesema, “ninapocheza soka, nina furaha, najiona mtu muhimu kwenye jamii na nafurahi kubadilishana mawazo.”

Ingawa vifaa vya michezo kama vile mipira na viatu ni adimu, bado soka imesalia mbinu muhimu ya kuondoa mawazo kwa wachezaji na watazamaji na njia ya kurejesha matumaini kuwa siku moja kupitia soka wanaweza kuchipua katika maisha.

“Nitawajibika kutunza dada zangu na wazazi wangu. Soka inaweza kunisaidia mustakabali wangu. Itanisaidia kupata marafiki. Natakuwa kuwe mchezaji bora wa soka ili nisaidie familia yangu. Mama yangu anahaha kutunza familia yetu nami nataka nimtunze,” amesema Patrick akiwa kwenye kambi hiyo ya michezo.

Familia ya Patrick ilikimbia mji wao wa Yei nchini Sudan Kusini miaka mitatu iliyopita na walitembea muda mrefu hadi kufika eneo salama nchini Uganda, nchi ambayo ni mwenyeji wa zaidi ya wakimbizi milioni 1, idadi kubwa ikiwa ni kutoka Sudan Kusini.

Kwa kuwa idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Sudan Kusini wana umri wa chini ya miaka 18, Stephen Abe ambaye ni mchezaji- kocha mwenye umri wa miaka 21 anasema, “siku  nzima unafikiria kuhusu wale uliowaacha na wale uliopoteza, lakini ukiwa uwanjani huo msongo unapotea.”

Kwa upande wao, Marco Bracco na Roberto Morosini ambao ni makocha wa Sampdoria wanaotoa mafunzo kwenye kambi hii, wanasema walitaka kurejesha matumaini na kuonesha mshikamano wao na vijana wapenda soka.

“Wakimbizi wanakbiliwa na matatizo mengi, kwa hiyo pengine kwa siku tatu wanaweza kujikita kwenye soka. Ilikuwa ni ndoto yetu ndogo na sasa tupo hapa na tuna furaha,” amesema Marco. 

Wadau wengine waliowezesha kambi hiyo ya siku tatu ni kamati ya olimpiki ya Uganda, shirikisho la soka la Uganda, na shirika la kiraia la kiitaliano, ACAV.

Akizungumzia mpango huo, afisa wa UNHCR nchini Uganda, James Bond Anywar amesema, “watoto wanapokuwa hawapo shuleni, hawana la ziada la kufanya kwenye makazi, kwa hiyo michezo inawafanya wawe kwenye harakati. Michezo inawasaidia pia kupata marafiki na kuendeleza amani.”

 

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud