Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia angalau zimepungua kidogo Yemen- Griffths

Mwananchi wa Yemen akisukuma mkokoteni wenye chakula cha msaada huko kwenye mji mkuu Sana'a. Mapigano yamesababisha raia wengi kutegemea chakula cha msaada (3 February 3019)
WFP/Annabel Symington
Mwananchi wa Yemen akisukuma mkokoteni wenye chakula cha msaada huko kwenye mji mkuu Sana'a. Mapigano yamesababisha raia wengi kutegemea chakula cha msaada (3 February 3019)

Ghasia angalau zimepungua kidogo Yemen- Griffths

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekutana kujadili ya kisiasa na kibinadamu nchini Yemen ambapo mjumbe maalum wa umoja huo kwa Yemen Martin Griffiths amesema ghasia kwenye majimbo sita nchini humo zimepungua kufuatia pande husika kwenye mkataba wa Hudaydah kupunguza mapigano licha ya kwamba utekelezaji wa mkataba huo haujawa kikamilifu.

Bwana Griffiths amesema miezi mitano kabla ya kutiwa saini kwa mkataba huo mwezi Disemba mwaka jana, zaidi ya raia 1,300 waliuawa kwenye mapigano, lakini miezi mitano baada ya kutiwa saini makubaliano, idadi ya vifo imepungua kwa asilimia 68.

Hata hivyo amesema bado ana wasiwasi mkubwa kuhusu mwendelezo wa mashambulizi na vifo miongoni mwa raia akisema kuwa, “hata hivyo ni dhahiri kuwa, kupungua kwa ghasia kunaendelea kuwa na manufaa kwa wakazi wa Hudaydah na watoa huduma za kibinadamu. Katika miezi ya karibuni, wajumbe wa kamati ya kujipanga upya Hudaydah wameendelea kushirikiana vyema na Jenerali Michael Lollesgaard juu ya mipango ya awamu ya kwanza na ya pili ya kupanga upya vikosi mjini humo.”

Wajumbe wa Baraza la Usalama wakimsikiliza Martin Griffith, mjumbe maalum wa UN kwa Yemen akihutubia kwa njia ya video kuhusu hali ya Yemen. (17 Juni 2019)
UN /Loey Felipe
Wajumbe wa Baraza la Usalama wakimsikiliza Martin Griffith, mjumbe maalum wa UN kwa Yemen akihutubia kwa njia ya video kuhusu hali ya Yemen. (17 Juni 2019)

Bwana Griffiths amesalia na matumaini kuwa makubaliano kati ya pande zote juu ya upangaji upya vikosi vyao mjini Hudaydah utafanikiwa kwa mujibu wa makubaliano yao kwenye mkataba wa Stochkholm ikiwemo mfumo wa utatu wa ufuatiliaji.

Mjumbe huyo maalum amesema, “pindi masuala ambayo hayajapatiwa ufumbuzi yatakapotatuliwa, utekelezaji wa pamoja utaanza na hivyo kuruhusu pande zote kuthibitisha masuala ya upangaji tena upya vikosi vyao.”

Amepongeza hatua za kujengeana imani kati ya pande husika huku akisema kuwa, “masuala ya uchumi kuhusiana na mapato ya bahari kama ilivyoainishwa kwenye mkataba wa Hudaydah yatapatiwa pia kipaumbele. Natumaini kuafikiana kwenye masuala hayo kutawezesha kuwalipa mishahara watumishi wa umma jimboni Hudaydah na kwingineko Yemen.”

Amezungumzia vile ambavyo serikali ya Yemen na kikundi cha Ansar Allah ambavyo kwa pamoja wamesisitiza kuwa suluhu ya kisiasa ndio pekee katika mzozo wa Yemen.

Mjumbe huyo amewakumbusha wajumbe wa Baraza la Usalama kuwa ni lazima watambue umuhimu wa kutatua mzozo huo hivi sasa kaw kuwa, “kadri mzozo unavyokomaa ndivyo itakuwa vigumu zaidi kuutatua sambamba na kurekebisha madhara ambayo yatakuwa yamejitokeza.”

Wafanyakazi wa UNHCR wakisambaza misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa ndani huko Aden nchini Yemen baada ya mvua kubwa kunyesha mjini humo tarehe 10 Juni 2019
© UNHCR/NMO
Wafanyakazi wa UNHCR wakisambaza misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa ndani huko Aden nchini Yemen baada ya mvua kubwa kunyesha mjini humo tarehe 10 Juni 2019

Hali ya Kibinadamu

Wajumbe pia walipata taarifa ya hali ya kibinadamu nchini Yemen kutoka kwa mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura, OCHA, Mark Lowcock.

Bwana Lowcock akawaeleza kuwa “leo ni mara yangu ya 15 kuhutubia Baraza hili na ni  hotuba ya 36 tangu mwaka 2015 uanze mzozo wa Yemen.”

Mzozo wa Yemen ni sawa na ‘simulizi ya Panyabuku’

Amefafananisha uzoefu wake kwenye suala la yemen ni sawa na mhusika mkuu wa kwenye filamu ya Hollywood ya ‘Siku ya Panyabuku” ambaye anakuwa amenasa kwenye eneo huku akijaribu kujinasua bila mafanikio na kila aamkapo anajikuta kwenye mtego ule ule.

Kwa mantiki hiyo amesema ingawa anaweza kuwa na jipya kuhusu Yemen lakini taswira kubwa ni ile ile kama aamkavyo Panyabuku na hivyo amesema, “leo nitakachofanya ni kuangalia nyuma na kuelezea ni nini kinahitajika ili kuwaondoa wayemen katika mtego waliomo.”

Historia

“Zaidi ya watu 70,000 wameuawa nchini Yemen tangu wameuawa tangu mwaka 2016 na kwamba ghasia inaweza kupungua eneo moja na kupamba moto eneo linguine,” amesema Lowcock.

Amesema kwa sasa kuna maeneo 30 ya uwanja wa vita Yemen, hali ambayo inathibtisha kuwa kama vita ikipungua eneo moja, wapiganaji wanaweza kuingia makundi mengine na kuendelea na vita.

“Mapigano yanazidi na si kupungua, watu zaidi ya 250,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani mwaka huu pekee. Idadi ya matukio ya mauaji au kujeruhiwa kwa watoto yameongezeka mara tatu kati ya robo ya mwisho yam waka jana na robo ya kwanza ya mwaka huu,” amesema Mkuu huyo wa OCHA.

Bwana Lowcock amesema sit u kwamba vita hiyo ni katili bali pia haina mshingi, “ingawa kila mtu anakubali kuwa hali ndiyo hivyo kupitia taarifa zao kwa umma, lakini bado vita inaendelea.”

Amesema kila mwezi wanatoa takwimu kuwa asilimia 80 ya wayemen au wananchi milioni 24 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi lakini bado hali si shwari huku miundombinu ya kijamii zikiwemo hospitali na shule zikiendelea kusambaratishwa.

Mtoto huyu pichani mwenye umri wa miezi miwili ni mkazi wa Hajjah, nchini Yemen na ana unyafuzi. Mzozo unaoendelea nchini Yemen unasababisha mamilioni ya watu wawe hatarini kukumbwa na baa la njaa.
WFP/Marco Frattini
Mtoto huyu pichani mwenye umri wa miezi miwili ni mkazi wa Hajjah, nchini Yemen na ana unyafuzi. Mzozo unaoendelea nchini Yemen unasababisha mamilioni ya watu wawe hatarini kukumbwa na baa la njaa.

Jinsi gani Yemen ijinasue kwenye mtego?

Hata hivyo amependekeza mambo matano ya kuitoa Yemen kwenye mtego wa sasa ambapo mosi ni mosi; sitisho la mapigano nchini kote; pili; pande zote kwenye mzozo ziwezesha huduma za binadamu  kufikia wahitaji bila vikwazo vyovyote.; tatu; kuhakikisha ombi la usaidizi kwa Yemen linakamilishwa akisema kuwa “mwaka huu tunahitaji dola bilioni 4.2 na hadi sasa tumepata dola 1.15 tu sawa na asilimia27.”

Kipaumbele cha  nne ni hatua endelevu za kuimarisha uchumi wa Yemen na tano ni kusongesha amani kwa mujibu wa makubaliano ya Stockholm.