Kudhibiti kuenea kwa jangwa ni hatua mujarabu kufanikisha SDGs- Guterres

Nchini Cameroon, matumizi ya ardhi  yasiyo endelevu yamesababisha kuenea kwa jangwa. (Februari 2019)
UN News/Daniel Dickinson
Nchini Cameroon, matumizi ya ardhi yasiyo endelevu yamesababisha kuenea kwa jangwa. (Februari 2019)

Kudhibiti kuenea kwa jangwa ni hatua mujarabu kufanikisha SDGs- Guterres

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametaka hatua za dharura zichukuliwe ili kulinda na kurejesha ardhi iliyomomonyoka sambamba na ongezeko la kuenea kwa jangwa duniani kama njia mojawapo ya kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu.

Bwana Guterres amesema hayo katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya kukabiliana na kuenea kwa jangwa hii leo, ambayo inaenda sambamba na maadhimisho  ya miaka 25 tangu kupitishwa kwa mkataba wa kimataifa wa kukabiliana na kuenea kwa jangwa.

Akifafanua hali ilivyo, Guterres amesema, “kila mwaka dunia inapoteza tani bilioni 24 za udongo wenye rutuba. Na mmomonyoko wa ardhi katika maeneo makavu unapunguza pato la ndani la taifa kwa asilimia 8 kila mwaka katika nchi zinazoendelea.”

Kwa mantiki hiyo amesema ni lazima kubadili mwelekeo wa sasa kwa kuwa, “kulinda na kuirutubisha ardhi na kuitumia vyema, kunaweza kupunguza uhamiaji wa kulazimishwa, kuimarisha uhakika wa chakula, na kuwa chachu ya ukuaji uchumi. Pina kunaweza kusaidia kushughulikia dharura ya kimataifa ya tabianchi,”

Akizungumzia siku ya leo, Ibrahim Thiaw, ambaye ni Mkuu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa wa kudhibiti kuenea kwa jangwa, UNCCD, amekumbusha kuwa maamuzi ya kila siku ni muhimu katika kuamua kudhibiti kuenea jangwa.

Watoto katika eneo la Merea nchini Chad wakipanda miti kama nija mojawapo ya kukabiliana na kuenea kwa jangwa nchini humo
UNDP Chad/Jean Damascene Hakuzim
Watoto katika eneo la Merea nchini Chad wakipanda miti kama nija mojawapo ya kukabiliana na kuenea kwa jangwa nchini humo

Amesema, tathmini ya sasa inaonesha kuwa hekta moja katika kila hekta nne ya ardhi yenye rutuba inakuwa haiwezi kutumika tena kutokana na mmomonyoko au kuenea kwa jangwa, na kwamba hekta tatu kati yanne zimebadilishwa kabisa matumizi yake ya asili.

Bwana Thiaw amesema katika mazingira hayo na kasi hiyo ambamo kwayo kuongeza uzalishaji wa chakula kwa asilimia 50 ilhali uharibifu wa ardhi an mabadiliko ya tabianchi vinapunguza mavuno ya mazao kwa asilimia 50, kunafanya suala la ulinzi na uhifadhi wa ardhi “liwe ni la kila mtu anayetaka kula, kunywa au kupumua.”

Siku ya kimataifaya kudhibiti kuenea kwa jangwa huadhimishwa tarehe 17 mwezi Juni kila mwaka ili kusongesha mbinu bora na manufaa ya kulinda ardhi kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Mataifa 196 na Muungano wa Ulaya ni wanachama wa UNCCD, ambapo kati ya hizo, nchi 169 zimeathiriwa na jangwa, mmomonyoko wa udongo au ukame.