Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola si dharura ya afya duniani, bali DRC na nchi jirani- WHO

Mhudumu wa afya akipima joto la mwananchi kwenye eneo la mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Uganda. Wahudumu wa afya kwenye kituo hiki wamekuwa wakichukua vipimo kubaini iwapo wananchi wana Ebola au la. (12 Feb 2019)
UNICEF/Jimmy Adriko
Mhudumu wa afya akipima joto la mwananchi kwenye eneo la mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Uganda. Wahudumu wa afya kwenye kituo hiki wamekuwa wakichukua vipimo kubaini iwapo wananchi wana Ebola au la. (12 Feb 2019)

Ebola si dharura ya afya duniani, bali DRC na nchi jirani- WHO

Afya

Kamati ya dharura ya shirika la afya duniani, WHO imetangaza kuwa mlipuko wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ni tishio la afya nchini humo na nchi jirani pekee.

Akitangaza uamuzi wa kikao cha dharura cha kamati hiyo kilichofanyika leo huko Geneva, Uswisi, Kaimu mwenyekiti wa kamati hiyo, Dkt. Preben Aavitsland amesema hatua hiyo inazingatia kuwa mlipuko wa sasa haukukidhi vigezo vitatu vya kanuni za afya za kimataifa za kuweza kuutangaza kuwa ni dharura ya kiafya duniani kote.

Hatua za kuchukua

Kwa mantiki hiyo amesema wametoa mapendekezo yanayopaswa kuzingatiwa na DRC na nchi jirani, mapendekezo ambayo ni pamoja na, “nchi zilizo hatarini ziboreshe mifumo yao ya kujiandaa kubaini na kushughulikia visa vilivyobainika kama ambavyo Uganda ilifanya. Uchunguzi dhidi ya Ebola kwenye maeneo ya mpakani na DRC uendelee na uboreshwe na uwe endelevu. WHO ifuatilie na kuchapisha maandalizi ambayo yanafanywa na nchi  jirani dhidi ya Ebola.”

Halikadhalika Dkt. Aavitsland amesema WHO iendelee kufuatilia mienendo inayoweza kuweka hatari ya kusambaa kwa Ebola na kwamba nchi zote ziweke uthibitisho wa dawa za kutibu Ebola kama njia ya kujiandaa kudhibiti ugonjwa huo.

Hata hivyo amesema kamati imevunjika moyo sana kwa kuwa “WHO na nchi zilizokumbwa na Ebola hazijapata rasilimali na fedha zinazotakiwa kudhibiti mlipuko wa sasa. Jamii ya kimataifa iongeze fedha na usaidizi kwa maandalizi dhidi ya Ebola huko DRC na nchi jirani.”

Amesema kutokea kwa visa vya Ebola na vifo Uganda ni kumbusho kwamba kadri mlipuko huu unaendelea DRC, kutakuwepo na hatari ya kusambaa nchi jirani.

Mhudumu wa afya anayehusika na ebola akimchunguza ugonjwa huo mtoto mchanga mwenye umri wa wiki moja kwenye hema maalum la kituo cha matibabu dhidi ya ebola huko Beni jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC Desemba 3, 2018
UNICEF/Guy Hubbard
Mhudumu wa afya anayehusika na ebola akimchunguza ugonjwa huo mtoto mchanga mwenye umri wa wiki moja kwenye hema maalum la kituo cha matibabu dhidi ya ebola huko Beni jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC Desemba 3, 2018

Ushirikiano kati ya DRC na Uganda ni siri ya mafanikio

Kaimu mwenyekiti huyo wa kamati ya dharura ya WHO amepongeza hata hivyo ushirikiano kati ya DRC na Uganda na mawasiliano kati nchi mbili hizo ambayo yamesaidia kudhibiti kusambaa zaidi kwa mlipuko.

Kamati pia imesisitiza suala la elimu kwa jamii hususan ya mipakani huko ikiomba Umoja wa Mataifa na wadau waratibiane ili kuimarisha usalama na kuweka mazingira bora kwa ajili ya operesheni za kudhibiti Ebola nchini DRC.

Hakuna vizuizi vya safari kwenda DRC

Kuhusu vizuizi vya safari, Dkt. Aavitsland amesema wamebaini kuwa si lazima kuweka vizuizi vya safari sambamba na uchunguzi kwenye viwanja vya ndege.

Kufuatia uamuzi huo, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus, akizungumza kutoka DRC amekubali uamuzi huo kuwa mlipuko wa sasa wa Ebola ulioanza nchini DRC mwezi Agosti mwaka jana si dharura ya umma duniani bali kwa taifa hilo la Maziwa Makuu na ukanda husika.

Tweet URL

 

Ebola ni dharura kwa familia na jamii zilizokumbwa na ugonjwa huo

Hata hivyo amekumbusha kuwa kwa jamii na familia zilizokumbwa na ugonjwa huo bado ni dharura kwa hiyo hatua hatua za kudhibiti ziendelee.

Dkt. Tedros amesema tayari amekutana na mamlaka za DRC pamoja na upande wa upinzani na wahisani kujadili jinsi ya kudhibiti Ebola na kesho atakwenda Goma na Butembo kukutana na wafanyakazi walio mstari wa mbele kukabili Ebola.

Kwa mujibu wa Dkt. Tedros, tangu mlipuko uanze mwezi Agosti mwaka jana hadi leo hii, watu 2108 wameambukizwa Ebola nchini DRC na kati yao hao 1411 wamefariki dunia.