Binti mwenye umri wa miaka 16 nchini Tanzania atengeneza Apu ya kusaidia wanawake wajawazito kufuatilia hali zao.

14 Juni 2019

Sauti za wanawake na wasichana na ujuzi katika sayansi, teknolojia na ubunifu ni muhimu katika kuleta suluhu katika dunia ya sasa ambayo inashuhudia mabadiliko ikiwemo mabadiliko haribifu, yanasisitiza mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la wanawawake yaani UN Women na lile la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO.

 

Wito huo umeitikiwa vema na Khatija Safi Juma msichana mwenye umri wa miaka 16 anayesoma kidato cha tatu katika shule ya sekondari Ndono wilayani Uyui, Tabora Tanzania aliyebuni ‘App’ ya kuwasaidia akina mama wajawazito.

Malongo Mbeho  mwandishi wa habari aliyejotolea kwa UN News amezungumza na msichana huyo na kwanza akamuuliza alipataje wazo hilo? "ni kutokana na maeneo ambayo tunaishi, na kuona kwamba akina mama wengi wanapata shida pale wanapokuwa wajawazito kwa kuwa hospital ziko mbali. Lakini pia kutokana na kutokuwa na uelewa zaidi kuhusu masuala ya afya, hicho ndicho kimenipelekea kubuni hiyo App. Na hiyo alianza tangu nilipoingia kidato cha kwanza kwani ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza kuishi vijijini na kushuhudia vifo.” Anaeleza Khatija.

Binti mwenye umri wa miaka 16 nchini Tanzania atengeneza App ya kusaidia wanawake wajawazito kufuatilia hali zao.
ITU
Binti mwenye umri wa miaka 16 nchini Tanzania atengeneza App ya kusaidia wanawake wajawazito kufuatilia hali zao.

Na kuhusu ni namna gani ‘App’ hiyo inafanya kazi, Khatija anafafanua,“ina sehemu ambayo inahifadhi taarifa za mwanamke kama ni mjamzito kuhusu ujauzito wake na hapo kutakuwa na sehemu ambayo inamkumbusha kuhusu tarehe za kwenda kliniki, lakini pia kuna sehemu za ushauri kwa akina mama kwa ujumla. Kuna pia vyakula anavyotakiwa kula na pia tumeandika athari zipi unaweza kuzipata usipoenda kliniki au kutofuata mlo ipasavyo, hivyo ndivyo tumeziweka.”

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, katika masomo ya ngazi ya juu takribani asilimia 30 pekee ya wanafunzi wa kike ndiyo wanachagua masomo yanayohusiana na sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati. Vile vile takwimu hizo zinabainisha kuwa wanawake watafiti  ni asilimia 30 pekee kote duniani.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter