Ndege zisizo na rubani zaokoa Maisha ya kusafirisha damu Rwanda:WHO

14 Juni 2019

Upatikanaji wa damu salama ni sehemu ya utekelezaji wa lengo la huduma za afya kwa wote lakini pia ni kipengee muhimu katika utendaji kazi wa mifumo ya afya kote duniani limesema leo shirika la afya ulimwenguni WHO katika maadhimisho ya siku ya uchangiaji damu duniani. 

Siku ya uchangiaji damu duniani ambayo kila mwaka huadhimishwa Juni 14 kwa mujibu wa WHO ni ya kuwashukuru mamilioni ya watu wanaojitolea kwa hiyari zawadi kubwa ya akiba katika maisha yao ambayo ni damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wengine lakini pia kuelimisha umuhimu wa uchangiaji damu katika jamii ili kuhakikisha watu na jamii zote wanapata fursa ya damu kwa gharama nafuu na kwa wakati.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni “damu salama kwa wote” na Rwanda ndio mwenyeji wa maadhimisho ya kimataifa kwa siku hiyo.

WHO inasema Rwanda imepiga hatua kubwa katika kutumia teknolojia mpya ili kuokoa Maisha ya watu wanaohitaji damu vijijini. Kwa miongo miwili iliyopita Rwanda imaimarisha huduma ya damu nchi nzima na kuongeza mara tatu kiwango cha uchangiaji damu kati ya mwaka 2000 na 20018. Mafanikio haya ya huduma Rwanda WHO inasema yamechangiwa na kutumia teknolojia bunivu kama ndege zisizo na rubani au drone kwa kusafirisha damu haraka kwa wanaohitaji.

Huduma ya kuongeza damu Rwanda.

Huduma ya kuongeza na kuchangia damu ilianza nchini Rwanda mwaka 1975 na tangu mwaka 1985 ilikuwa ni kwa hiyari na bila malipo yoyote. Mauaji ya kimbari ya 1994 yalisambaratisha vibaya miundombinu na mifumo ya afya Rwanda lakini serikali ilitoa kipaumbele katika kujenga upya huduma ya uongezaji damu kwa kutambua ni jinsi gani ilivyo muhimu kuwa na fursa ya upatikanaji wa damu katika kuokoa maisha. Hivyo nchi hiyo ikachukua hatau mbalimbali kuimarisha usalama na upatikanaji wa damu nchi nzima njia ambazo WHO inasema zimesaidia kupunguza vifo vya watoto kwa theluthi mbili kati ya mwaka 2000 na 2015 na vifo vya kina mama  wajawazito kwa robo tatu.

Kutokana na juhudi hizo leo hii kituo cha taifa cha uongezaji damu (NCBT) kinatoa damu ya kutosha na salama kwa wagonjwa wote wanaoihitaji. Na lengo hili limefikiwa kupitia vituo 541 vya kudumu vya ukusanyaji damu na vituo 5 vya kikanda vya usambazaji damu ambavyo vinahudumia vituo vya afya 66 vya uongezaji damu.

Rwanda inavyokabili changamoto za ufikishaji damu

Moja ya changamoto kubwa iliyokuwa ikiikumba Rwanda katika kufikisha damu kwa wanaohitaji hususani vijijini ni miundombinu kwani ni taifa la milima na barabara mbovu. Lakini sasa inatumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani au drones ziitwazo “zipline” ambazo zinakata muda wa kusafirisha damu hiyo kutoka saa 4 hadi dakika 15 kwa baadhi ya maeneo. Akizungumzia umuhimu wa hatua hivyo waziri wa afya wa Rwanda Dkt. Diane Gashumba amesema “kila sekunde unayoongeza katika kuokoa maisha ni muhimu sana , tulipotambua kwamba zipline zitakuwa suluhu hatukusita.”

Huduma hii inapendwa sana hata na walionufaika nayo kama mama Alice Mutimutuje ambaye anasema “nilikuwa naziona drone zikiruka na kufikiria kwamba huu ni wendawazimu , hadi pale drone hiyohiyo ilipookoa maisha yangu.”

Kuchangia damu

Lakini teknolojia kama hizo bila wachangiaji damu inayohitajika hazina maana. Tangu 1985 sera ya Rwanda ni kwamba uchagiaji damu ni wa hiyari bila malipo na inatolewa kwa wagonjwa wanaoihitaji bure bila malipo. Na wachangiaji nchini humo wana arri ya kuchangia miongoni mwao ni Euphasie Uwase Maneno anayesema “kila wakati niña furahi kuokoa maisha ya mtu hata kama ni mtu ambaye simfahamu kwa sababu katika utamaduni wetu tunaamini kwamba kuwa binadamu ni kufanya jambo jema kwa mtu bila kutarajia shukran.

Hata hivyo shirika la WHO linasema fursa ya kupata damu salama sio utamaduni kwa kila nchi, katika siku hii ya uchangiaji damu linatoa wito wa upatikanaji wa damu salama kwa wote , likisema Rwanda ni mfano ambao unapaswa kuigwa endapo dunia itahitaji kuwa na damu salama ya kutosha na bidhaa zingine za damu kwa ajili ya kila anayehitaji , ikiwaasa watu kujitolea damu leo ili kuokoa maisha.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud