Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Unyanyasaji wa kingono dhidi ya wazee unatakiwa kuwekwa wazi- Kornfeld-Matte

Muathirika wa ukatili wa kingono mjini Goma DRC.
Picha ya UN/Marie Frechon (Maktaba)
Muathirika wa ukatili wa kingono mjini Goma DRC.

Unyanyasaji wa kingono dhidi ya wazee unatakiwa kuwekwa wazi- Kornfeld-Matte

Haki za binadamu

Kuelekea siku ya kimataifa ya kuelimisha kuhusu unyanyasaji dhidi ya wazee inayoadhimishwa Juni 15 kila mwaka, mtaalamu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za wazee Rosa Kornfeld-Matte leo mjini Geneva Uswisi ametoa tamko akieleza kuwa unyanyasaji wa kingono na ubakaji dhidi ya wazee ni jambo ambalo halijadiliwi mara nyingi ingawa lipo na ni la kweli.

Aidha ameeleza kuwa unyanyasaji mwingi dhidi ya wazee unafanyika bila kufahamika na hauripotiwi hata pale ambapo kuna ishara za tahadhari.

Taarifa ya Bi Kornfeld-Matte imeendelea kueleza kuwa unyanyasaji wa kingodo na ubakaji kwa wazee bado ni mwiko na unafanyika kimyakimya na kadri muda unavyozidi kusogea, tatizo hili linategemewa kuongezeka kwa kasi.

“Hata hivyo bila data, takwimu za kutosha, na utafiti kuhusu manyanyaso kwa wazee, hatutakuwa na hata makadirio ya ukubwa wa tatizo.” Taarifa ya Bi Kornfeld imetahadharisha.

Mojawapo ya changamoto alizozitaja mtaalamu huyo wa Umoja wa Mataifa ni kuwa unyanyasaji wa kingono kwa wazee unafikiriwa kufanywa na watu wa mbali na familia za wazee hao wakati cha kusikitisha ni kuwa unyanyasaji mwingi unafanywa na wanafamilia, ndugu na watu wengine ambao wako katika nafasi za kuwahudumia wazee hao.

Pia kuna changamoto nyingi zinazowakwamisha wazee kuweza kuripoti visa vya kunyanyswa kutokana na hali zao zinazosababishwa na umri mkubwa na hivyo kunakuwa na mazingira magumu ya utunzaji na baadaye upatikanaji wa ushahidi.

Na kwa hivyo Bi Kornfeld-Matte ametoa wito wa kuchukua hatua, “tunapaswa kuwa makini zaidi na kuripoti visa vinavyohisiwa kuwa vya unyanyasaji wazee.”

 

TAGS: Rosa Kornfeld-Matte, Wazee, Unyanyasaji wazee.