Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakuu wa nchi na wadau wa maendeleo wakutana kuimarisha ASTF.

ASTF imewanufaisha maelfu ya wakulima, wanawake na vijana katika nchi 41 za Afrika
©FAO/Andrew Esiebo
ASTF imewanufaisha maelfu ya wakulima, wanawake na vijana katika nchi 41 za Afrika

Wakuu wa nchi na wadau wa maendeleo wakutana kuimarisha ASTF.

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Wakuu wa nchi, mawaziri na wadau wengine wa maendeleo wanakutana mjini Malabo nchini Guinea ya Ikweta kuangazia jukumu la Mfuko wa mshikamano kwa Afrika (ASTF).

Ujumbe wa FAO katika ufunguzi wa mkutano huo umesema mfuko wa mshikamano kwa Afrika, ASTF, kielelezo madhubuti cha mshikamano miongoni mwa nchi za bara la Afrika kuboresha kilimo na uhakika wa chakula unahitaji kuunda ushirikiano mkubwa na kuchunguza mifumo bunifu ya uwezeshaji kifedha ili kukabiliana na changamoto zinazolikabili bara la Afrika.

FAO ilianzisha ASTF, mfuko unaoendeshwa na kuongozwa na Afrika, kwa ajili ya Afrika ili kusaidia mikakati na mipango ya maendeleo ya Afrika. Tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2013, ASTF imewanufaisha maelfu ya wakulima, wanawake na vijana katika nchi 41 za Afrika kwa kufadhili miradi mbalimbali ambayo imesaidia kukuza fursa za ajira vijijini, kuongeza uzalishaji wa kilimo, na kuzalisha njia mpya za kipato.

Maria Helena Semedo ambaye ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO anasema, “leo tunatakiwa kujenga kwenye mwendo na mafunzo ambayo tumejifunza katika hii miaka ya hivi karibuni. Njaa na utapiamlo bado ni changamoto kubwa barani Afrika na vinaweza kushughulikiwa kupitia ujitoleaji mpana. Kwa sababu hiyo, ASTF inaanzisha ushirikiano mpya hasa na washirika wa maendeleo, benki na sekta binafsi. Ili kuifikia kikamilifu ndoto ya ASTF tunahitaji kikundi muhimu cha wachangiaji.”