Mfumo wa ulimwengu wa ajira ubadilike, kwani sasa umeongeza pengo la wenye nacho na wasio nacho- Macron

11 Juni 2019

Mabadiliko makubwa  na ya msingi yanahitajika katika mfumo ajira duniani ikiwemo kuweka kiwango cha chini ya mshahara ili kushughulikia ongezeko la pengo kati ya walio nacho na wasio nacho.

Hiyo ni kauli ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa wakati akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la shirika la kazi duniani, ILO mjini Geneva, Uswisi hii leo.

Katika hotuba yake ya dakika 45, Macron amesema kitendo cha watu wachache kujinufaisha na utandawazi na kujilimbikizia utajiri kimeanzisha sheria za porini ambazo zimefungua mlango wa uzawa, chuki dhidi ya wageni na watu kukata tamaa kuhusu demokrasia.

Uchumi wa soko ni kandamizi

“Huu uchumi wa soko ambamo kwao tunaishi si wa kijamii kama ambavyo tulitaka kushuhudia baada ya Vita Vikuu vya Pili vya duniani na unasababisha kuwepo kwa watu wachache kujilimbikizia kipato na kuongezeka kwa makundi makubwa kumiliki kampuni,” amesema Macron.

Hata hivyo amesema kuwa tatizo hilo linaweza lisionekane kuwa ni janga kubwa kwa sababu “waathirika ni watu wasio na sauti, wametawanyika na hawajaungana, na hatujaona vita ikiibuka kutokana na tatizo hili lakini kuna janga.”

Akitaka mshikamano wa kimataifa na kuondokana na janga la sasa, Rais Macron ametaka kuwepo kwa kima cha chini cha mshahara kwa nchi za Muungano wa Ulaya akisema kuwa, “tukishindwa kufanya hivyo tunahatarisha kuona wafanyakazi wa nchi za EU wakiondoka nyumbani na kwenda kusaka ajira kwingineko ambako kuna uhakika wa kima cha chini cha mshahara kama vile Ufaransa na Ujerumani.”

Watoto na watu wazima kutoka Romania wakifanyakazi katika eneo la kutupa taka jirani na makazi ya Nadezhda nchini Bulgaria. Familia hizi zinakosa fursa za ajira, ambayo ndio kauli mbiu ya ripoti ya mwaka huu ya ILO kuhusu mtazamo wa ajira na mwenendo Duni
UNICEF
Watoto na watu wazima kutoka Romania wakifanyakazi katika eneo la kutupa taka jirani na makazi ya Nadezhda nchini Bulgaria. Familia hizi zinakosa fursa za ajira, ambayo ndio kauli mbiu ya ripoti ya mwaka huu ya ILO kuhusu mtazamo wa ajira na mwenendo Duni

Ajira si bidhaa- Merkel

Mapema Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alipongeza falsafa ya ILO kuwa dhima ya uchumi ni kuhudumia watu na si watu kuhudumia uchumi.

Pamoja na kupongeza jitihada za ILO za kufanya ulimwengu wa ajira kuwa pahala salama na penye haki, Bi. Merkel amesema chombo hicho kinahitajika zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule.

Ametaja suala la ajira kwa watoto akisema, takribani watoto milioni 152 duniani kote wanatumikishwa na milioni 73 kati yao wako kwenye ajira hatarishi.

 “Hii haikubaliki kabisa na lazima tushirikiane tuondokane na tatizo hili” akisema katika dunia ya sasa ni lazima kuhakikisha ukuaji wa uchumi unaleta maendeleo ya kijamii kwa kila mtu wakiwemo watoto.

Kansela Merkel amegusia utandawazi akisema kuwa  umesababisha ukosefu wa haki ambapo  wahamiaij milioni 232 wanafanya kazi kwa kutumikishwa kwenye sekta kama vile ujenzi na kazi za ndani, huku watu wengine milioni 700 ni maskini licha ya kwamba wanafanya kazi.

 “Ajira si bidhaa” amesema Bi. Merkel wakati akisoma azimio la ILO la mwaka 1944 akisema kuwa umaskini kwenye eneo moja unatishia ustawi kwenye eneo lingine kwa hiyo ni lazima kushirikiana.

Waziri Mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la ILO hii leo huko Geneva, Uswisi. (Juni 11, 2019)
ILO webcast
Waziri Mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev akihutubia mkutano wa Baraza Kuu la ILO hii leo huko Geneva, Uswisi. (Juni 11, 2019)

Mfumo wa kimataifa ni tete- Medvedev

Akiunga mkono hoja ya ushirikiano baina ya mataifa, Waziri Mkuu wa Urusi, Dmitry Medvedev amesema mfumo wa sasa wa kimataifa ni tete kupita kiasi.

Ametaka uelewa wa kina wa changamoto pahala pa kazi hivi sasa akigusia magari yasiyohitaji dereva ambayo teknolojia yake itaengua mamilioni ya madereva wa teksi na malori.

Ametaka pia mahitaij ya wafanyakazi  na jamii yazingatiwe akisema kuwa kwa kuyapuuza, madhara yake ni makubwa kuliko.

 

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter