Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtu kwao, wakimbizi waliokimbia machafuko Sudan Kusini wanaendelea kurejea nyumbani

Amani ya kudumu nchini Sudan Kusini ni muarobaini kwa mustakhbali wa watoto kama hawa nchini humo ambao sasa haki zao za msingi zinasiginwa.
UNMISS
Amani ya kudumu nchini Sudan Kusini ni muarobaini kwa mustakhbali wa watoto kama hawa nchini humo ambao sasa haki zao za msingi zinasiginwa.

Mtu kwao, wakimbizi waliokimbia machafuko Sudan Kusini wanaendelea kurejea nyumbani

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakati hali ya kupungua kwa mizozo ikishuhudiwa nchini Sudan Kusini tangu kutiwa saini kwa makubaliano mapya ya amani mwezi Septemba mwaka jana wa 2018,, familia nyingi zimekata kauli ya kurejea nyumbani. Priscilla Lecomte na taarifa zaidi.

Ni shamra shamra za kuanza safari ya kuondoka eneo la kuhifadhi raia na kuelekea nyumbani eneo la Jonglei nchini Sudan Kusini, wafunga safari na wanaosalia wakipungiana salamu za kuagana.

Safari imeanza asubuhi baada ya jua kuchomoza huku wasafiri wakiwa wamefungasha virago vyao wakielekea moja kwa moja hadi Uwanja wa ndege.

Watu takriban 86 wengi wao wakiwa wanawake na watoto wamesafirishwa kwa helikopta ya Umoja wa Mataifa kuelekea Yuai eneo la Jonglei nchini Sudan Kusini, ambako wamekaribishwa kwa shangwe na vigelegele na ndugu na marafiki.

Mama huyu akiwa amebeba mwanae ni mmoja wa wakimbizi wa ndani waliorejea, anasema kuwa “nilikuwa natamani kurejea tangu mwaka jana lakini sikuweza, lakini sasa namshukuru Mungu kwamba nipo hapa Yuai na watoto wangu. Ninaamini kwamba madhila yangu sasa yamefika ukomo.”

Takriban watu 3,000 waliokuwa wamesaka hifadhi katika maeneo ya ulinzi wa raia ya Umoja wa Mataifa wakati wa mzozo walielezea nia yao ya kutaka kurejea nyumbani, utaratibu ambao uliendeshwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS, Shirika la Umoja huo la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na wadau.

Tunakutana na mnufaika mwingine wa mpango huo.

“Ningependa kushukuru Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha miaka sita ambapo walikuwa wanatuhifadhi katika vituo vya kuhifadhi raia kuanzia mwaka 2013 hadi 2019. Ni kazi nzuri ambapo wanalinda waathirika hadi pale wanapoweza kujitegmea.”

Kwa upande wa walinda amani ambao wanashuhudia kurejea kwa familia ambazo wamezilinda tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe mwezi Disemba mwaka 2013, ni raha baada ya karaha kama anayosema Kevin Mutua Mutune, afisa wa ulinzi na maridhiano wa UNMISS.

“Kwa kuwarejesha katika mazingira ambamo wanayapenda na damilia zao pia ni namna ya kutoa ulinzi. Wantoka kutoka hali ambapo ni kizuizi lakini wakirejea nyumbani wako huru kushirika shughuli mbali mbali ikiwemo kilimo, uvuvi, biashara na hata wengine kurejea shule kwa hiyo tunajaribu kuwawezesha kuendelea na maisha yao.”

Idadi ya watu 86 waliorejea ni ishara ya wachache wa mamilioni ya wakimbizi na waliofurushwa ambao wameanza safari ya kurejea nyumbani wakati huu ambapo kunashuhudiwa amani kote nchini na mustakabali bora na ambao walikuwa wanatamani unageuka kutoka kuwa ndoto hadi hali halisi.