Usawa wa jinsia ni muhimu katika kulinda bahari zetu-Guterres

8 Juni 2019

Ikiwa leo ni siku ya bahari duniani, maudhui yakiwa jinsia na bahari, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anataka dhima ya wanawake katika matumizi  ya rasilimali za bahari kupigiwa chepuo zaidi.

Katika ujumbe wake wa siku ya leo, Bwana Guterres anasema mara nyingi uhusiano wa jinsia na uhifadhi na utunzaji wa rasilimali za bahari hupuuzwa wakati huu ambapo bahari zinachafuliwa, matumbawe yanababuliwa licha ya umuhimu wa rasilimali hizo kwenye uhai wa binadamu na sayari ya dunia.

“Athari za uchafuzi wan a mabadiliko ya tabianchi kweney bahari hukumba kwa kiasi kikubwa wanawake. Kwa muda mrefu , wanawake wameshindwa kunufaika ipasavyo na rasilimali za bahari,” amesema Katibu Mkuu.

Ameongeza kuwa wanawake ni nusu ya nguvu kazi inayohusika na uvuvi na mavuno ya samaki wa baharini na wale wafugwao lakini bado ujira wao ni mdogo kuliko wanaume.

Kama hiyo haitoshi amesema, “wanawake mara nyingi wanatengwa na kufanya kazi zisizo na stadi za kutosha na zisizotambuliwa kama vile kuchakata samaki, na wananyimwa haki ya uamuzi kwenye masuala ya uvuvi.”

Bwana Guterres amesma hali ni hivyo hivyo kwenye sekta kama vile usafirishaji melini, utalii wa pwani na sayansi ya viumbe vya bahari ambako amesema ni nadra sana kusikia sauti za wanawake.

Kwa mantiki hiyo katika kuhakikisha matumizi endelevu ya bahari na zaidi ya yote kuhakikisha kuwa yana manufaa kwa pande zote, Katibu Mkuu anapigia chepuo kuondokana na ukosefu wa usawa wa jinsia kwenye matumizi ya rasilimali za bahari.

Idadi ya wanawake kwenye bonde la Ziwa Chad huko Afrika Magharibi wanaojihusisha na uvuvi inazidi kuongezeka na sasa wanavua na hata kupaa ili waweze kuuza na hatimaye kupata kipato.
UN News/Dan Dickinson
Idadi ya wanawake kwenye bonde la Ziwa Chad huko Afrika Magharibi wanaojihusisha na uvuvi inazidi kuongezeka na sasa wanavua na hata kupaa ili waweze kuuza na hatimaye kupata kipato.

“Kuondokana na ukosefu wa usawa wa jinsia ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yahusianayo na masuala ya bahari. Lazima tuhakikishe tunatokomeza mazingira yasiyo salama na kuweka mazingira ambamo kwayo wanawake wana jukumu sawa katika kusimamia shughuli zihusianazo na matumizi ya rasilimali za bahari,” amesema Bwana Guterres.

Amesihi serikali, mashirika ya kimataifa, jamii na watu binafsi kusongesha usawa wa jinsia na haki za wanawake na wasichana kama moja ya hatua muhimu ya kuona mchango wao katika kukabiliana na changamoto zinazokabili bahari hivi sasa.

UNESCO NAYO YAPAZA SAUTI

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO linasisitiza umuhimu wa wanawake kushiriki zaidi katika ngazi zote za matumizi ya rasilimali za baharini kuanzia uvuvi hadi  uhifadhi wa bahari.

Audrey Azoulay ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO amesema ingawa wanawake wanashiriki kwenye ngazi hizo hivi sasa bado sauti zao hazisikiki katika ngazi ya juu ya uamuzi.

Amenukuu ripoti ya kamisheni ya UNESCO inayosema kuwa wanawake ni asilimia 38 tu ya idadi yote ya wanasayansi wa masuala ya bahari ilhali, “wanawake ni asilimia 50 ya nguvu kazi kwenye huduma za uvuvi, lakini mishahara yao inaendelea kuwa midogo kuliko ya wanaume.”

“Ili kuweka mwelekeo wenye uwiano wa kibinadamu na kuchagiza mbinu bunifu za kulinda bahari zetu ni lazima tuweke usawa wa jinsia na pia kuweka mazingira kwa wanawake na wasichana kuwa na mchango wao kwenye mabadiliko dhati ya matumizi ya bahari,” amesema Bi. Azoulay.
 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter