Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 115 wa kiume walioa wakiwa watoto-UNICEF

Barubaru katika manispaa ya Gujara kwenye jimbo la Rautahat nchini Nepal wakiwa katika mchezo wa kuigiza wa ndoa za umri mdogo ulioandaliwa na UNFPA na UNICEF
UNICEF/Kiran Panday
Barubaru katika manispaa ya Gujara kwenye jimbo la Rautahat nchini Nepal wakiwa katika mchezo wa kuigiza wa ndoa za umri mdogo ulioandaliwa na UNFPA na UNICEF

Watoto milioni 115 wa kiume walioa wakiwa watoto-UNICEF

Haki za binadamu

Takriban watoto wavulana na wanaume milioni 115 walioa wakiwa watoto kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF.

Ripoti hiyo  ya kwanza kabisa ya aina yake kuhusu watoto  inaonesha kuwa wavulana walioa wakiwa na umri mdogo na kwamba mtoto mmoja kati ya watano alioa kabla ya kutimiza umri wa miaka 15.

Ripoti hiyo iliyokusanya takwimu kutoka nchi 82 inatanabaisha kwamba ndoa za utotoni miongoni mwa watoto wa kiume zimekita mizizi katika nchi nyingi kote ulimwenguni kuanzia kusini mwa Jangwa la Sahara, Amerika Kusini na Carribea , kusini mwa Asia, mashariki mwa Asia na Pasifiki.

Akizungumzia ripoti hiyo, mkurugenzi mkuu wa UNICEF, Henrietta Fore, amesema, “ndoa hizo zinawapora utoto wao, mabwana harusi watoto wanalazimika kuchukua majukumu ya watu wazima ambayo huenda hawako tayari kuyamudu. Ndoa za mapema huwasababishia  kuwa wazazi mapema na changamoto ya kukidhi mahitaji ya familia, inakatisha fursa zao za elimu na za kazi.”

Kwa mujibu wa takwimu za UNICEF, Jamhuri ya Afrika ya Kati ina idadi kubwa ya ndoa za utotoni miongoni mwa wavulana ikiwa ni asilimia 28 ikifuatiwa na Nicaragua yenye asilimia 19 na Madagascariliyo na asilimia 13.

Makadirio mapya yanaonyesha idadi kamili ya watoto wa kike wanaoolewa na wa kiume wanaooa inafika milioni 765. 

Idadi ya wasichana wanaoolewa ni msichana mmoja kati ya kila watano walio na umri wa miaka 20 hadi 24 na waliolewa kabla ya kutimiza miaka 18 ikilinganishwa na mvulana mmoja kati ya thelathini.

UNICEF imesema licha ya kwamba ukubwa, sababu na athari za ndoa za utotoni miongoni mwa wasichana imetathminiwa, utafiti mdogo umefanyika kuhusu ndoa za mapema miongoni mwa watoto wa kiume.

Hatahivyo, watoto walioko hatarini zaidi kuolewa mapema wanatoka katika kaya maskini, wanaishi vijijini na wana viwango vya chini vya elimu.

Kwa mantiki hiyo Bi. Fore amesema, “wakati tukielekea maadhimisho ya miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mkataba wa kimataifa wa haki za watoto, ni muhimu kukumbuka kwamba kuoza wavulana na wasichana utotoni ni kinyume na haki zilizoorodheshwa kwenye maktaba huo.

Aidha ameongeza kwamba, “kwa kufanya itafiti zaidi, uwekezaji na uwezeshaji, tunaweza kutokomeza ukatili huo.”