Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maldives kukaguliwa iwapo inatekeleza haki za kitamaduni

Mtazamo wa Maldives kutoka angani
Picha ya maktaba
Mtazamo wa Maldives kutoka angani

Maldives kukaguliwa iwapo inatekeleza haki za kitamaduni

Utamaduni na Elimu

Mtaalamu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za kitamaduni Karima Bennoune jumapili hii itaanza ziara ya siku 10 nchini Maldives kwa lengo la kutathmini utekelezaji wa haki za kitamaduni nchini humo.

Taarifa iliyotolewa mjini Geneva, USwisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, imesema kuwa hii itakuwa ni ziara ya kwanza ya mtaalamu huru wa haki za binadamu nchini humo tangu 2013 na ya kwanza kufanywa na mtaalamu wa haki za kitamaduni kwenye taifa hilo la Kusini mwa Asia.

Bi. Bennoune amesema “kwa kuzingatia hali ya kipekee ya Maldives, nitatathmini pia sera zilizotungwa kupunguza tishio la madhara ya mabadiliko ya tabianchi kwa tamaduni na urithi wa utamaduni nchini humo na jinsi utamaduni na ubunifu vinatumiwa kukabiliana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi.”

Kwa mantiki hiyo amesema anatarajia kujifunza jinsi Maldives inaelewa suala la watu kupata haki zao za kitamaduni na jinsi juhudi za kuhakikisha suala hilo zinaheshimu haki za binadamu ikiwemo zile za kitamaduni.

Mtaalamu huyo pia anapanga kuchunguza athari za misimamo mikali katika mtu kufurahia haki za kitamaduni na jinsi watu wanafurahi nafasi yao kama wananchi bila kubaguliwa.

Akiwa nchini humo atatembelea visiwa kadhaa na kukutana na mamlaka kuu na za mashinani pamoja na kuzungumza na watu mbalimbali wanaofanya kazi kwenye nyanja za utamaduni, wakiwemo wasanii, wanazuoni na pia atakuwa na mazungumzo na mashirika ya kiraa na wawakilishi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa.

Bi.Bennoune atawasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa baadaye.