Usalama wa chakula ni jukumu la kila mtu- FAO/WHO

6 Juni 2019

Kuelekea maadhimisho ya kwanza kabisa duniani ya siku ya kimataifa ya chakula kesho Juni 7, shirika la afya ulimwenguni, WHO limetaka kuimarishwa zaidi kwa juhudi za kuhakikisha kuwa chakula ambacho kinaliwa ni salama.

Taarifa ya WHO iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema kuwa  hatua hiyo ni muhimu kwa sababu kila mwaka watu milioni 600 duniani kote wanaugua ilhali wengine 420,000 wanafariki dunia baada ya kula chakula kilichoharibiwa na bakteria, virusi, vimelea au dutu zenye kemikali.

Kando mwa hayo, chakula hicho kinadumaza maendeleo katika nchi nyingi za kipato cha chini na kati ambazo hupoteza takribani dola bilioni 95 kila mwaka kutokana na watu hao kushindwa kufanya kazi kwa sababu ya kuugua, ulemavu utokanao na vyakula visivyo salama.

Ni kwa kuzingatia athari hizo, WHO pamoja na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO ambayo ndio yanaratibu siku hii yametoa mapendekezo matano ya kuhakikisha chakula kina usalama.

Mapaendekezo hayo ni pamoja na serikali kuhakikisha chakula kinapaswa salama hivyo wakulima na wazalishaji watumie mbinu bora. Chakula kihifadhiwe salama hivyo wafanyabiashara wahakikishe usalama kinaposafirishwa, hifadhiwa na kuandaliwa.

Utupaji hovyo wa chakula ni adui mkubwa wa vita dhidi ya njaa
FAO/Jonathan Bloom
Utupaji hovyo wa chakula ni adui mkubwa wa vita dhidi ya njaa

Walaji nao wana jukumu kwa kuwa wanatakiwa wakipate kabla hakijaharibika, wapate taarifa sahihi kuhusu lishe na athari za magonjwa zihusianazo na chakula husika.

Kwa upande wake serikali na wadau washrikiane kuhakikisha chakula ni salama.

Akizungumzia siku hii yenye ujumbe kuwa usalama wa chakula ni jukumu la kila mtu,  Mkurugenzi Mkuu wa FAO, José Graziano da Silva amesema awe mkulima, msambazaji, mchakati au msafirishaji wa chakula, kila mtu ana jukumu kwa kuwa hakuna uhakika wa chakula bila usalama wa chakula.

Ni kwa mantiki hiyo WHO na FAO wanashirikiana kusaidia nchi kuzuia, kusimamia na kuchukua htaua za muda mrefu kwenye mnyororo mzima wa uzalishaji chakula ambapo wanashirikiana na wazalishaji, wauzaji, mamlaka za usimamizi, mashirika ya kiraia kuona usalama wa chakula kiwe kinaagiza kutoka nje au kinazalishwa ndani ya nchi.

Kwa mujibu wa mashirika hayo, uwekezaji katika elimu ya mlaji kuhusu usalama wa chakula umesaidia kupunguza magonjwa yahusianayo na sumu au vijidudu kwenye chakula na hivyo kurejesha uwekezaji wa kila dola 10 iliyowekezwa.

 

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter